Articles by "NGORONGORO"
Showing posts with label NGORONGORO. Show all posts

 MAKAMISHNA Wasaidizi Waandamizi wa Uhifadhi wanawake kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wapo nchini Indonesia kushiriki mkutano wa mtandao wa wanawake maafisa waandamizi wa Polisi na vyombo vingine vya usalama unaofanyika nchini humo.

Makamishna hao wanaongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Salma Chisonga, ambapo wanatarajiwa kushiriki katika majadiliano na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya ulinzi, uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Mkutano huo wa siku tano umewakutanisha wanawake kutoka vyombo mbalimbali vya usalama kutoka nchi tofauti duniani kwa lengo la kujadili fursa na changamoto zinazowakabili wanawake katika vyombo vya usalama pamoja na taasisi zinazolinda rasilimali za nchi.

Aidha, ushiriki wa makamishna hao unatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kubadilishana uzoefu na mataifa mengine kuhusu namna ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika ulinzi, uhifadhi wa rasilimali na usimamizi wa maeneo ya utalii.

Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano na mitandao ya wanawake katika vyombo vya usalama duniani, huku ukitoa nafasi ya kujifunza mbinu na uzoefu mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za kiusalama na uhifadhi.


 Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa Malaigwanani ,wazee na kina mama maarufu wapatao 33 kutoka kata 11 za ndani ya eneo la hifadhi Ngorongoro ili kuwajengea uwezo wa kutambua fursa mpya za kiuchumi.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia huduma za jamii bi Gloria Bideberi amesema lengo la semina hiyo ni kuhakikisha Malaigwanani na wazee hao wanapata elimu ya kutosha kuhusu ujasiriamali na namna ya kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao.

Bi. Gloria alieleza kwamba elimu hiyo itakwenda sambamba na ziara za kujifunza kwa vitendo, ambapo washiriki watatembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa bidhaa ikiwemo kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za maziwa Tanga Fresh kilichopo Mkoani Tanga ili kujifunza namna bidhaa zinavyozalishwa, kuendelezwa na kufikishwa katika masoko.

“Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa wananchi hawa wanapata elimu ya kutosha na kuwawezesha kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa bidhaa ili kujifunza kwa vitendo zaidi,” alisema Gloria

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuimarisha ushiriki wa jamii katika maendeleo endelevu ya eneo la Hifadhi Ngorongoro.











Rika la Erumeruasi katika jamii ya Watemi, Kata ya Oldonyosambu, Tarafa ya Sale wilayani Ngorongoro, limepongezwa kwa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Oldonyosambu chenye thamani ya sh ,milioni 305.411, hatua inayodhihirisha namna mila na tamaduni zinavyoweza kutumika kuchochea maendeleo na kuboresha huduma za jamii.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Hamza Husein Hamza, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, amesema juhudi hizo ni mfano wa kuigwa kwa jamii nyingine, akisisitiza kuwa mila na tamaduni zinapounganishwa na maendeleo zinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

 Alisema serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za jamii zinazolenga kuboresha huduma za msingi huku akisisitiza katika kuhakikisha afya ni muhimu kwa jamii Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ilichangia sh, milioni 80 katika ujenzi wa kituo hicho, huku akilitaja Rika la Erumeruasi kuwa miongoni mwa makundi yaliyotumia misingi ya mshikamano na uwajibikaji wa kijamii kuimarisha amani, usalama na maendeleo. 

Katika harambee iliyoambatana na sherehe hizo, wananchi na wadau walichangisha sh, milioni 184.493 kwa ajili ya mahitaji ya kituo hicho, ikiwemo vifaa tiba na vitendanishi.

Kituo hicho kinatarajiwa kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, hususan wanawake wajawazito ambao kwa muda mrefu walilazimika kwenda Digodigo au Engaresero kwa ajili ya kujifungua, hatua hiyo inaonesha kuwa mila ya kushirikiana na kuchangia maendeleo inaweza kuzaa matokeo yenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, hasa katika huduma muhimu kama afya.

Sherehe hizo pia ziliambatana na makabidhiano ya uongozi na majukumu ya kijamii kutoka Rika la Erumeruasi kwenda Rika la Erumashili, huku Pius Maroseck akikabidhiwa jukumu la kuongoza rika hilo.

 Makabidhiano hayo yanaakisi umuhimu wa mila za jamii ya Watemi (Wasonjo) katika kurithisha majukumu, heshima, amani na mshikamano kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, huku vijana wakihimizwa kutumia misingi hiyo kuendeleza maendeleo ya jamii.









 


Wahadzabe ni kabila linalopatikana mkabala na ziwa Eyasi pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro na habari za maisha yao zimehifadhiwa katika makumbusho ya Urithi Jiopaki liyopo Karatu Mkoani Arusha.

Pamoja na mabadiliko ya ulimwengu na elimu kutolewa lakini kabila hili bado haliamini katika tohara kwa kijana wa kiume, kwao hiyo ni mwiko wakiamini binadamu anastahili kuwa kama alivyozaliwa.

Sababu kubwa ya kutokutahiriwa ni kuwa ukitahiriwa unapunguza nyama ya binadamu na kuizika wakati binadamu huyo akiwa hai, imani ni kwamba huwezi kata sehemu yoyote ya mwili wa binadamu aliye hai

Vilevile kabila  hili linaamini kwamba mwanaume akitahiriwa hupunguza ukubwa na utaalam wa mambo na kufanya  mwili wako kuwa na mapungufu hata wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Katika kuhakikisha kwamba mwanaume anakuwa na nguvu za kutosha wakati wa kushiriki tendo la ndoa hulazimika kula mizizi inayopatikana porini , matunda, asali ikiwa fresh na nyama pori ambayo inachomwa au kuchemshwa supu.

Kutokana na kutokutahiriwa Wahadzabe wanaamini kwamba miili yao huwa na nguvu ya kupambana na mnyama yoyote porini na hiyo ndiyo heshima ya mwanaume kamili ambaye hata anapochumbia kutaka kuoa hupimwa kwa uwezo wa kuwinda na kuleta chakula cha familia.

Hii ni sehemu ya maajabu ya maisha makabila wanaunda Ngorongoro Global Geopark ambapo licha ya Wahadzabe kuendelea kuishi katika ukanda huo lakini taarifa zao zinapatikana katika makumbusho ya Urithi Geopark.

Karibu Nyumbani Ngorongoro upate mshangao wa maajabu na uzoefu usiosahaulika.

 


Wakati Maonesho ya Nanenane yakiendelea kupamba moto katika maeneo mbalimbali nchini, Hifadhi ya Ngorongoro imeendelea kutanua mbawa zake na kuonesha vivutio vya utalii mubashara kupitia mitandao ya kijamii na luninga kubwa iliyofungwa kwenye banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.

Watalii wanaotembelea maonesho hayo wameshuhudia vivutio vya wanyama mbalimbali kama Faru, Tembo, Pundamilia, Swala, Nyumbu, Simba wakiwa honeymoon, na makundi ya Nyati yakiwa yanajimbwafai katika maeneo yao ya asili.

Akiwa katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Meneja wa Idara ya Utalii na Masoko wa Ngorongoro SACC. Mariam Kobelo, ameeleza kuwa Ngorongoro imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii na kuboresha huduma ili wageni waweze kushuhudia vivutio mubashara na kufurahia huduma zinazotolewa na Ngorongoro.

“Ngorongoro ikiwa ni eneo la kipekee, tumejipanga kuendelea kutumia teknolojia za kisasa kufikia watu na kuona maajabu na simulizi adhimu za kipekee.

 Katika jamii ya Kimaasai, maisha ya mwanaume hupitia hatua mbalimbali za kimila zinazoonyesha ukuaji, Miongoni mwa hatua hizo muhimu ni kufanyiwa sherehe inayojulikana kwa jina la Orkiteng le Sirit ikimaanisha ni mwisho wa ujana na kuingia uzeeni.

Katika hatua hii ambapo mtu anatawazwa kuingia rika la uzee, wazee wa jamii hiyo huchagua Dume la rika ambalo lina afya njema na lililohasiwa tangu utoto wake, dume hili siku ya shughuli ndio hutolewa mwanzo kwenye boma lenye  Ng’ombe wengi na kumwagiwa maziwa kisha hunyongwa hadi kufa. 

Sherehe ya Orkiteng le Sirit , si sherehe ya kawaida bali ni tukio la heshima kubwa linalofanyika kwa kufuata mila na desturi za kale zilizorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kwa jamii ya Kimaasai, ni hatua ya ukamilifu wa mwanaume na uthibitisho kwamba ametimiza majukumu yake ya kifamilia na kijamii, kufanyiwa sherehe hii hakuangalii umri ila inazingatia jinsia kwa kuwa anayefanyiwa sherehe hii ni mwanaume pekee, vigezo vinavyoangaliwa ili mwanaume afanyiwe sherehe hii, ni lazima awe ameoa, awe na watoto wa kike na kiume na awe mtu mwema na maadili katika jamii.

Akizungumza wakati wa sherehe hiyo, Alaigwanani wa kabila la kimasai Maningo Rinjo amesema viongozi wa mila wa ukoo kama (Laizer, Mollel, Laitayo, Ngidong’i) ndio wenye jukumu la kumchagua dume atakayechinjwa baada ya kujiridhisha kuwa ana sifa zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kimaasai ili kutekeleza jukumu hilo la kijamii ambalo linahudhuriwa na ndugu wote wa familia na jamii yote ya wamasai inayozunguka Kijiji hicho. 

“Si kila dume anaruhusiwa kutumika katika sherehe hii, sisi viongozi wa mila hukagua na kuthibitisha sifa zake kabla ya kutoa ruhusa ya kuchinjwa, dume wa kutekeleza sherehe hii lazima awe amehasiwa tangu utotoni, hajawahi kumpanda dume jike, pembe zake ziwe zimenyooka bila kupinda mithili ya pembe za mbogo, asiwe mgonjwa na sifa zingine za ndani ambazo viongozi wa kimila ndio huzichunguza kwa undani,” alisema Alaigwanani Maningo Rinjo.

Alaigwanani Olonyori Lemoyan kutoka Ukoo wa Laizer Kata ya Nainokanoka Ngorongoro alisisitiza kuwa si kila mwanaume anastahili kufanya sherehe ya Orkiteng le Sirit, moja wa masharti muhimu ili mwanaume afanyiwe tukio hilo kuwa

na familia yenye watoto wa kike na kiume, awe na mali na uelekeo wa maisha, mtu anayejali watu na awe ni rafiki wa ukoo wake na jamii inayomzunguka pamoja na kupata ridhaa ya ukoo wake kufanya sherehe hiyo. 

“Orkiteng le Sirit ni heshima kubwa katika jamii ya Kimaasai. Mwanaume lazima awe ametimiza wajibu wake wa kifamilia kwa kupata watoto wa kike na wa kiume. Bila kutimiza sharti hilo, hawezi kufikia hatua hii muhimu ya maisha,” alisema Alaigwanani Olonyori Lemoyan.

Wakati wa sherehe hizo baada ya dume kunyongwa na kutolewa nyama zake, mwanaume anayehitimu (anayepandishwa rika) pamoja na mke wake na mama yake mzazi wanatakiwa hukalia utumbo wa dume hilo kama ishara ya kuaga rasmi ujana na kuingia katika hatua ya uzee. Kitendo hicho hubeba maana kubwa ya kiutamaduni na kuashiria mwanzo wa jukumu jipya ndani ya jamii na kuachana na usharobaro na mambo yote ya ujana.

Baada ya taratibu hizo kukamilika, rika la Korianga huungana na mwenzao aliyeingia hatua ya uzee timilifu huimba nyimbo za furaha na heshima huku wakielekea bomani, wakimpongeza mwenzao kwa kufikia hatua hiyo adhimu. Nyimbo hizo huashiria kukubalika kwake rasmi katika kundi la wazee na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mila, desturi na maamuzi yanayohusu ustawi wa jamii.

Orkiteng le Sirit si tu sherehe ya kuchinja dume laa hasha, ni alama ya mafanikio ya maisha, uwajibikaji wa kifamilia na heshima ya kuwa mzee katika jamii ya Kimaasai. Hatua hii ni urithi wa kipekee unaoendelea kuunganisha vizazi na kuhifadhi utamaduni wenye thamani kubwa kwa jamii hiyo.







 


Washiriki zaidi ya 300 wameshiriki mbio fupi za kilomita 5 katika  bonde la Olduvai Ngorongoro kwa lengo la kutangaza vivutio vya asili vya Olduvai na Laetoli ambapo historia ya Binadamu wa Kale ilianzia.

Akizungumza kwa Niaba ya Kamishna wa Uhifadhi kwenye tukio hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko Mariam Kobelo ameeleza kuwa

Ngorongoro kwa kushirikiana na Cape to Cairo Marathon imefanya mbio hizo ili kuonesha utajiri wa utalii wa asili, historia, urithi wa utamaduni na  mambo kale uliopo Olduvai na Laetoli kama Nyumbani kwa asili ya Binadamu. Ameongeza kuwa Ngorongoro ni Nyumbani kwa Nyumbu wanaohama kwa kuwa pumzi ya kwanza ya ndama kupigwa mhuri kabla ya kuhamia maeneo mengine safari yao huanzia Ndutu Ngorongoro.

"Ngorongoro ni Nyumbani kwa asili ya binadamu kisayansi, Ni nyumbani kwa Nyumbu wanaohama kila mwaka, ni nyumbani kwa Spinshi ya Ndege zaidi ya 500, ni nyumbani kwa Wanyama wakubwa watano, kiufupi eneo la Ngorongoro ni Nyumbani kwa mkusanyiko wa Vitu vingi ndio maana tunawaambia wadau wote ndani na nje ya Nchi kuwa Wonders Are Calling" ameongeza Kamishna Kobelo.

 Mkurugenzi wa Cape to Cairo Arusha International Marathon, Timothy Mdinka ameeleza kuwa lengo la mbio hizo ni kutangaza mazao mapya  ya Utalii yaliyopo Tanzania na Bara la Africa kwa Ujumla kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo  Michezo kama mbio ambayo imefanyika leo Olduvai pamoja na marathon ya Cape to Cairo itakayofanyika tarehe 31 Mei, 2026.

Mbio hizo zimejumuisha wadau mbalimbali wakiwepo Ngorongoro, Cape to Cairo international Marathon, Karatu Runners,  Amani Collection, CRDB, UNDP, NHIF,  Diplomatic and Tourism Police Arusha

 


Kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watalii wa ndani kutembelea hifadhi ya Ngorongoro hii ikimaanisha wanarudi nyumbani eneo ambalo ndilo pekee lenye ushahidi wa kisayansi usiotiliwa shaka kuwa ndio chanzo cha binadamu wa kale.

Safari hii ni zamu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) chini ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa  hilo Usharika wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam Rev, Dr. Elliona Kimaro aliyeongoza kundi la wanaume 300 kutoka mikoa mbalimbali nchini kutembea Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai (Urithi Geopark) na vituo vya hifadhi vilivyopo Ngorongoro 

Akiwa na Ujumbe huo Dkt.  Kimaro amesema makundi mbalimbali kuhamasika kufanya utalii wa Ndani wanavutiwa na vitu mbalimbali ikiwemo kushuhudia uumbaji wa Mungu, kuona na kujifunza Chanzo cha asili ya Mwanadamu katika bonde la Olduvai na Laetoli, kuona Ikolojia ya hifadhi pamoja na utunzaji wa Mazingira kama vitabu vitakatifu vinavyohimiza.

"Tumekuja Nyumbani Ngorongoro kwenye asili ya Mwanadamu tukiwa na kundi la wanaume 300,  tumeshuhudia uumbaji wa Mungu, utunzaji wa Ikolojia, Mazingira, Misitu Wanyama wa kila aina ya vyote vilivyoumbwa kwa mfano wa Mungu" alisema  Dkt. Kimaro.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inawarudisha nyumbani binadamu wote ili kushuhudia asili yao ambapo binadamu alianza kutembea na kufanya shughuli zake kwa miguu miwili.






 Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc kutoka mataifa ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Falme za Kiarabu na Rwanda wamerejea Nyumbani Ngorongoro kushuhudia asili ya mababu zao iliyosheheni vivutio vya utalii vya Wanyamapori, Malikale, Urithi wa Utamaduni na Jiolojia vilivyopo Ngorongoro ambayo ni Kivutio bora cha Utalii Afrika mwaka 2023 na 2025.

Wakiwa ndani ya hifadhi hiyo maarufu duniani, Wakurugenzi hao  wamefurahishwa na mandhari, uoto wa asili, wanyamapori pamoja na huduma bora za utalii zinazotolewa ndani ya hifadhi na kusisitiza kuwa uzoefu walioupata umeacha alama inayowafanya kurudi tena na familia zao.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Prof. Neema Mori amesema ujumbe huo umeichagua Ngorongoro kuwa sehemu yao ya mapumziko kutokana na upekee wake usiofananishwa na eneo lolote duniani  kwa kuwa Ngorongoro si tu kivutio cha Utalii bali ni hazina ya historia, utamaduni na asili inayoishi.

Akiwa na Ujumbe huo Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Utalii na Masoko Mariam Kobelo amesema kuwa  Ngorongoro ndio eneo lenye ushahidi wa kisayansi na Kimazingira kuwa binadamu wa kwanza alisimama kwa miguu yake miwili zaidi ya miaka Milioni 3.6 iliyopita huku hifadhi hiyo ikipambwa na wanyama wakubwa watano "Big Five", Spishi za Wanyama mbalimbali, Ndege, maua na mimea.




 


Maadhimisho ya siku ya Urithi wa Dunia Afrika yaliyofanyika katika Makumbusho ya Urithi Jiopaki mjini Karatu tarehe 5 Mei, 2026 yameyakutanisha  wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ikiwa na lengo la kuwarithisha kizazi kipya historia na elimu ya urithi na utamaduni.

Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Dkt Lameck Karanga amesema uwepo wa makabila hayo, historia yao pamoja na kuenzi tamaduni zao ni utajiri mkubwa kwa Tanzania na kutoa wito kwa wadau na jamii kwa ujumla kuendelea kulinda maeneo ya urithi wa dunia na kuibua maeneo mapya yatakayoingizwa katika orodha ya Urithi wa Dunia ili kuongeza thamani ya ubora wa kipekee ulimwenguni (Outstanding Universal Value) na kuvutia wageni wengi zaidi.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii Ngorongoro Joas Makwati ameeleza kuwa mamlaka itaendelea kuongeza juhudi za kulihifadhi eneo la Ngorongoro ambalo ni urithi wa dunia na  kultangazia zaidi kama eneo pekee lenye Ushahidi wa kisayansi  kuhusu historia ya binadamu unaoeleza kuwa binadamu kwa kuthibitishwa na ugunduzi wa masalia ya binadamu wa kale na zana za mawe zilizopatikana katika bonde la Olduvai. 

Kwa upande wake Naibu Katibu wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania Dkt. Khamis Said ameeleza kuwa tangu Tanzania ijiunge na UNESCO imepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuridhia mikataba kumi (10) ya  UNESCO,Kuwepo kwa Hifadhi Hai za Mwanadamu na Mazingira  sita (6)  na Kuwepo kwa maeneo saba (7) ya urithi wa Dunia.

Kauli mbiu ya siku ya urithi wa dunia kwa mwaka huu ni “Kusherekea siku ya Urithi wa Dunia na kukuza Viongozi wa baadaye”. (Celebrating Africa’s Heritage, Mentoring the Leaders of Tomorrow).



Kutoka Pemba, Unguja, Mji mkongwe, Bagamoyo, Kondoa, Magofu ya kilwa, paa la mlima kilimanjaro na maeneo mengine ya Tanzania, wadau wa urithi wa dunia wamekutana katika Makumbusho ya Urithi Geopark Karatu Mkoani Arusha yanayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  kwa lengo la kuadhimisha   Urithi wa Dunia Afrika yaliyoanza leo tarehe 04/05/2026 hadi tarehe 05/05/2026.

Wakiwa katika jengo la makumbusho ya Urithi Geopark Wadau hao wameelezwa jinsi Ngorongoro ilivyo ni utajiri wa urithi wa dunia kutokana na uumbwaji wake uliotokana na mlipuko wa volcano zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita na kutengeneza kasoko iliyokusanya asili, uhai wa binadamu, mifumo ya ikolojia, na ustawi wa viumbe mbalimbali.

Katika  taarifa yake kwa vyombo vya habari Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru amewashukuru wadau wote hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la  Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)   kwa kuipa fursa Ngorongoro kuandaa na kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu.

Wadau wa urithi wa duania wakiwa katika Makumbusho ya Urithi Geopark walipata fursa ya kuelezewa kuhusu uthibitisho wa wasomi unaoeleza wazi historia ya chimbuko la binadamu wa kale aliyepatikana katika bonde la olduvai  takribani milioni  2 iliyopita na ushahidi wa Nyanyo za binadamu wa kale  katika eneo la Laetoli takribani miaka  3.6 iliyopiTa ambapo binadamu hao walitembea kwa miguu miwili.

Taasisi zinazoshiriki maadhimisho hayo ambazo zinasimamia maeneo ya urithi wa dunia ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Mamlaka ya Uzimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za misitu Tanzania (TFS), pamoja na wawakilishi wa maeneo ya urithi wa dunia kutoka Zanzibar.

 Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru leo tarehe 9 Aprili, 2026 amepuliza rasmi Kipenga cha shindano la mwezi mmoja la Safari Field Challenge akisisitiza kwamba Ngorongoro ni nyumbani kwa kila binadamu kutokana na chimbuko la historia linalobainishwa kisayansi.


Akizindua shindano hilo Kamishna Badru amewashukuru washiriki nane (8) wa shindano hilo kwa kuitika wito wa Ngorongoro na kuwaeleza kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ni zaidi ya Kreta hasa kutokana na kuwa na utamaduni, asili, chimbuko la binadamu wa kale, siri ya Binadamu na maisha yake, Nyayo za Laetoli zenye umri za zaidi ya miaka milioni 3.6, mchanga unaohama, kushuhudia pumzi ya kwanza ya Nyumbu eneo la Ndutu, kuona Wanyama wakubwa watano katika eneo moja, mlima Lolmalasian ambao wa tatu kwa urefu Tanzania, misitu, mimea na ndege mbalimbali.

“Karibuni Ngorongoro ambapo ni nyumbani kwa sisi sote, mtapata uzoefu ya maajabu mbalimbali, kuyahisi, kuyaishi, kufurahia, kuyahadithia na kuwasaidia kupata ujuzi ambao utawafanya muwe mabalozi wazuri kuwaelezea watu wengine mkusanyiko wa maajabu yaliyoko Ngorongoro” Alisema Kamishna Badu.

Kamishna Badru amewapa changamoto washiriki wa shindano hilo kuwa watundu wa kuifahamu Ngorongoro, kuisemea Ngorongoro kwa mtazamo mpya wa sauti moja ambapo kwa kushirikiana na Azam Media hadithi, historia, maajabu ya Ngorongoro itasimuliwa na kufika pembe nne za dunia kuwa Ngorongoro sio kivutio cha utalii pakee bali ni Nyumbani kwa kila Binadamu ambapo historia yao ilianza.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Huduma za Utalii na masoko Mariam Chuma Kobelo amewaeleza washiriki wa Safari Field Challenge kuwa Tanzania ina vitu vingi vya Kujivunia,lakini Ngorongoro kuna vingi zaidi na kuwasisitiza washiriki wa shindano hilo kwenda kujifunza, kuifahamu na kuisimulia Ngorongoro kuwa ni zaidi ya Kasoko ya Ngorongoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tanzania Tour Guide Fondation (TTGF) Mosses Njole ameleza kuwa washiriki wote 8 wako timamu na wamejiandaa kikamilifu kushiriki shindano hilo na kuwapongeza Ngorongoro kwa kuwa wadhamini wakuu na wadau wengine wakiwepo Azam Media ambayo imekuwa sehemu ya kusimulia maajabu ya Ngorongoro.








 


Mwenyezi Mungu akitaka jambo litokee hutokea ndivyo ilivyotokea, uumbwaji wa Kasoko ya Ngorongoro zaidi ya miaka milioni 2.5 iliyopita ambapo mlima mrefu uligeuzwa kuwa bonde la Ngorongoro.

Wanafunzi wa madrasa kutoka jimbo la Kondoa mkoani Dodoma pamoja na walimu wao wameshuhudia uwezo huo wa Mwenyezi Mungu walipotembelea hifadhi ya Ngorongoro katika ziara iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo mheshimiwa Dkt Ashatu Kijaji (Mb)

Afisa Mhifadhi Mkuu na mkuu wa makumbusho ya Urithi Geopark Dkt. Agnes Gidna aliwaeleza wanafunzi na waalimu hao kuwa mlipuko mkubwa wa volcano uliugeuza mlima mkubwa uliokuwepo eneo hilo zaidi ya miaka milioni 2.5 iliyopita na kuwa kreta hii ni kudhihirisha wazi kwamba kwa Mungu hakuna kubwa.

Akizungumza kwa niaba ya kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Gloria Bideberi amempongeza mbunge wa jimbo hilo Dkt. Ashatu Kijaji ambaye pia ni waziri wa maliasili na Utalii kwa kusimamia sekta hiyo kwa vitendo ambapo ujio wa wanafunzi hao utaongeza jitihada za kutangaza utalii wa ndani.

Kiongozi wa Ujumbe huo Katibu wa Idara ya Elimu ofisi ya mbunge wa jimbo la Kondoa Ayoub Sogoi amesema ziara hiyo imedhihirisha kwa vitendo mafunzo wanayopata vijana hao kutoka madrasa na shule za msingi na sekondari.

 


Anajulikana kwa jina la Utani Profesa kutokana na uwezo mkubwa wa kujua vitu vingi katika hifadhi ya Ngorongoro katika utumishi wake wa miaka 34, ni mwanamke shupavu kuelekea siku ya wanawake tarehe 8 Machi, 2026

Tukio la kusisimua na hatari katika maisha yake ni tarehe 6 Machi 2020 Kreta ya Ngorongoro kwenye utekelezaji wa majukumu yake, ghafla Faru akamkimbiza bila yeye kujua ambapo alijaribu kutumia mbinu za medani alizofundishwa jeshini kujinasua lakini bahati mbaya alishambuliwa ingawa baadaye aliweza kuokolewa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.

Kamanda huyu wa Uhifadhi anaadhimisha siku ya wanawake duniani akiendelea kuchapa kazi na mara nyingi utamkuta kreta akifanya shughuli za uhifadhi, utafiti, sensa za wanyamapori na kupambana na mimea vamizi bila woga.

Ngorongoro tunampa maua yake kwa kuwa uzoefu ni mama wa Maarifa hivyo yeye kama Chanda chema tunamvika Pete anapotimiza miaka 6 ya tukio la Faru.

 


Mjua kwao hapotei njia, na mwenda pole hajikwai, unaweza ukafikiri utani kumbe inaelekea ni hivyo wale wote wanaopambana Kariakoo, Gaza, Teheran na kwingineko inaaminika kuwa asili yao ni Bonde la Olduvai lililoko eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Bonde la Olduvai linafahamika kama eneo la kipekee duniani kupatikana masalia ya jamii za binadamu wa kale na zana za mwanzo za mawe yanayowakilisha hatua muhimu za awali katika chimbuko la binadamu kuanzia miaka milioni 2 iliyopita hadi sasa.

Kupitia eneo hili ndio ulimwengu ulipoanza kujua historia ya safari ya mabadiliko ya mwanadamu baada ya ugunduzi wa fuvu maarufu la Zinjanthropus mwaka 1959 ambalo lilibadilisha uelewa na mtazamo wa wanasayansi kuhusu mchango wa Tanzania katika masuala ya asili ya binadamu.


Bonde Olduvai limehifadhi visukuku, historia na chimbuko la binadamu katika mtiririko uliokamilika.