Maelfu ya wananchi wa jimbo la Monduli wameonyesha nguvu yao na imani kwa Izack Joseph Copriano maarufu Kadogoo wakati alipochukua fomu ya kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tukio hili limeonyesha wazi kwamba Kadogoo anashikilia nafasi ya pekee katika mioyo ya wananchi wa jimbo hilo.

Wanawake wa Kimasai waliokuwepo walimshukuru Mungu na pia kumpongeza Kamati Kuu ya CCM kwa uamuzi wa kurejesha jina lake na kukata la Fred Lowasa. Wamesema Kamati Kuu imefanya haki bila kuzingatia umaarufu au asili ya familia, na kumchagua mtoto wa mkulima aliyejitoa kwa wananchi.

“Kadogoo aliumia sana aliposhindwa katika kura za maoni, na sasa tumeona haki imefanyika. Tupo hapa kumunga mkono kwa dhati,” alisema mwanamke mmoja wa kimasai.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe, alisema Kadogoo ni kiongozi anayejali wananchi wake. “Monduli imepata kiongozi anayejitoa kwa wananchi na ambaye anafahamu changamoto zao. Kadogoo ni mchapa kazi,” alisema Mwaisumbe.

Wananchi wamesema mgombea huyo amefika kila kata, kushughulikia migogoro ya ardhi na kero mbalimbali za wananchi, jambo linaloonesha kwamba ni kiongozi wa vitendo. Maelfu waliovalia rangi za kimasai na kushiriki katika msafara walimsindikiza Kadogoo hadi ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wakionyesha imani yao na mshikamano wao na mgombea wao wa CCM.

Tukio hili limeonyesha nguvu ya wananchi wa Monduli na namna wanavyohamasika kuunga mkono viongozi wao wa vitendo. Kadogoo sasa anaingia rasmi katika mbio za ubunge akiwa na nguvu ya kishindo ya wananchi waliomchagua na kumpa shukrani kwa kazi zake zilizotimiza mahitaji yao.










Share To:

Post A Comment: