Na John Walter-Manyara


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka ameelezea kushangazwa na ukimya wa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika kuelezea mafanikio ya Serikali na kusema wengi wao wapo kimya na kwamba kufanya hivyo ni kutomtendea haki Rais Samia.

Shaka amesema hayo leo Jumamosi Mei 14, 2022 Mjini Babati katika mkutano wa ndani wa kujitambulisha mbele ya Wanachama wa CCM, kama Mlezi mpya wa Chama hicho kwa Mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda .

“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya kote nchini mna jukumu la kuyaeleza mafaniko ya Serikali ya Mama Samia, sasa hivi mpo kimya hamumtendei haki Rais wetu, katika utafiti wangu miaka miwili iliyopita kila RC na DC alikuwa akitoa taarifa za mafanikio ya Serikali kinyume na hali ilivyo sasa" Amesema Shaka

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake Rais Samia amefanya makubwa kana kwamba amekaa miaka mitano ikiwemo kuifungua Tanzania kiuchumi na kidiplomasia.

"Rais Samia ni kinara wa demokrasia katika ukanda huu wa Afrika Mashariki hilo liko wazi lazima tuyaseme mafanikio hayo, tangu aingie madarakani amechukua hatua kadhaa za kulainisha uhasama na kuponya vidonda" amesisitiza
Share To:

Post A Comment: