Bibi Fatuma Lwande na Mjukuu wake Mwajuma Said wakisafusha ndoo ili kuchota maji Mto Kombe uliopo kijiji cha Lwande kwa matumizi ya nyumbani.
Bibi Fatuma Lwande wa kijiji cha Lwande akisafisha ndoo ili kuchota maji mto Kombe kwa matumizi ya nyumbani.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Alex Odena akiangalia Jenereta ambayo itatumika kusukuma maji kuingia kwenye tenki la maji kijiji cha Lwande.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Alex Odena akiangalia Jenereta ambayo itatumika kusukuma maji kuingia kwenye tenki la maji kijiji cha Lwande.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi,Mhandisi Alex Odena akifafanua jambo kuhusu Mradi wa Maji Lwande.
Zainabu Mohamedi wa kijiji cha Sagasi akielezea furaha aliyonayo kwa kupelekewa maji na RUWASA.


Na Selemani Msuya, Kilindi


WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga umetumia Sh.milioni 504 za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kumaliza kero ya maji kijiji cha Lwande na Sagasi.

Fedha hizo ni sehemu ya mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba ili kuhakikisha Sera ya Maji inayotaka kila mwananchi anachota maji kwa umbali wa mita 400.

Hayo yamesemwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Alex Odena wakati akizungumza na waandishi wa habari walikuwa wanatembelea miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za ustawi Sh.milioni 504.

Amesema RUWASA wamelazimika kupeleka mradi huo kwenye kijiji cha Lwande baada ya chanzo cha maji kilichopo kuwa na maji ya uhakika na salama.

Mhandisi Odena amesema mradi huo ambao ni kwanza tangu kijiji kuanzishwa utahusisha usambazaji wa bomba kilometa 15.5, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 100,000 na vituo saba ambavyo hadi sasa vimeshakamilika.

“Tumetumia zaidi ya Sh.milioni 500 kutekeleza mradi huu wa Lwande ambao utanufaisha wananchi 4,611 wa vijiji viwili vya Lwande na Sagasa na utaongeza upatikanaji wa maji Kilindi hadi kufikia asilimia 36.6 kutoka asilimia 35 iliyopo kwa sasa,” amesema.

Meneja huyo amesema pia baada ya mradi huo kukamilika Kilindi itaongeza vijiji vinavyopata maji safi na salama hadi kufikia 43 kati ya 102.

Mhandisi Odena amesema mradi huo unaenda kuwatua ndoo kichwani wakina mama hali ambayo itachochea shughuli za kilimo, biashara na kijamii kupewa kipaumbele.

Odena amesema mradi huo umetekelezwa kwa ushirikishaji wananchi wa Lwande ambao wamepata ajira za muda na wengine watapatab za kudumu kama kuendesha mtambo wa kupandisha maji.

Meneja huyo wa RUWASA Kilindi amesema ina changamoto ya vyanzo vya maji, hivyo wanaendelea kutafuta vyanzo vingine ili kuhakikisha dhamira ya Serikali vijijini maji kupatikana kwa asilimia 85 inatimia.

Akizungumzia miradi hiyo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary amesema miradi ya maji mkoani hapo inagharimu zaidi ya Sh.bilioni 6.7 na itanufaisha wananchi 80,000.

Mhandisi Omary amesema zaidi ya vijiji 21 vitanufaika na fedha hizo katika majimbo 12 ya uchaguzi ya mkoa huo, hivyo lengo la mkoa kufikisha maji vijijini asilimia 85 na mijini asilimia 95 litatimia ifikapo 2025.

Diwani wa kata ya Lwande Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga, Hassan Mwengo amesema mradi huo umekuja wakati muafaka na kuahidi kuulinda kwa nguvu zote ili uwe endelevu.

Mwengo amesema ukosefu wa maji safi na salama kupitia bomba kulikuwa kunawapa wakati mgumu kunadi sera zao kwa kuwa wananchi wengi walikuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwande, Abdallah Gumbo amesema maendeleo ya kijiji chao yalikuwa yanadidimia kutokana na changamoto ya maji, hivyo ni imani yao kuwa maendeleo yatakuwa.

Mwananchi Ramadhani Kimweri wa kijiji cha Lwande amesema mradi huo wameupokea kwa shangwe kwa sababu tangu mwanzo wameshirikishwa, hivyo wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwakumbuka baada ya miaka 60 ya kupitia wakati mgumu kwenye eneo la maji.

“Wananchi wa Lwande ni wakulima na wafugaji, hivyo walikuwa wanatumia muda mrefu kutafuta maji, ila ujio wa mradi huu ni wazi kuwa tumekombolewa kiuchumi na kijamii.

Lakini pia kilichofanyika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 147 hadi 150, hivyo CCM imesafisha njia ya 2025,” amesema.

Kwa upande wake Bibi Fatumba Lwande (60) amesema changamoto ya maji inasababisha atumie muda wa saa mbili kufuata maji, hivyo uamuzi wa RUWASA kuwapelekea maji bombani ni wa kupongeza.

“Natuamia muda mwingi kufuata maji huku mtoni, unaona nimekuja huku na vitukuu, kwani siwezi kuwaacha, tunateseka sana,” amesema.

Mwajuma Said ambaye ni mjukuu wa Bibi Fatuma amesema kutokana na shida ya maji kijiji kwao analazimika kufuata maji mbali huku akiwa mjamzito, hali ambayo sio salama kwake na mtoto.

“Sina cha kusema tofauti na kumchukuru Rais Samia, kwani mateso haya ambayo mama wajawazito tumepitia naamini yanafikia mwisho,”amesema.

Naye Amina Mbezeni wa kijiji cha Sagasi amesema wanashukuru kupata maji safi na salama hali ambayo itawaondolea changamoto ya magonjwa mbalimbali.

Zainab Mohammed amesema matarajio yao ni kupitia mradi huo kijiji chao kitapata maendeleo kwa haraka, huku usafi wa mazingira ukiongezeka.

Naye Mkandarasi wa mradi huo, Enock Chengula amesema wanashukuru Serikali kuwapatia mradi huo ambao umewezesha wananchi zaidi ya 50 wamepata ajira.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: