Na. Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Wizara ya Fedha imebeba matumaini ya Serikali na Wananchi katika kuhakikisha kuwa inatafuta fedha za kuendeleza ujenzi wa miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
Mhe. Balozi Omar, amesema hayo katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Wizara ya Fedha (Treasury Square), jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Menejimenti na Wafanyakazi wa Wizara hiyo, baada ya kuwasili katika Ofisi hizo akiambatana na Naibu Mawaziri wake wawili, Mhe. Mshamu Ali Munde na Mhe. Laurent Deogratius Luswetula.
Alisema kuwa Wizara inatakiwa kuweka mikakati na mipango madhubuti ya kutafuta rasilimali za ndani kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha miradi mbalimbali pamoja na kuweka sera bora za fedha zitakazosaidia kuyawezesha makundi mbalimbali wakiwemo ya vijana kupata ajira na kufanya biashara.
Alisema kuwa Wizara ya Fedha ndio moyo wa Serikali kwa maendeleo ya nchi hivyo Menejimenti na Wafanyakazi wote wanapashwa kujipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana lakini pia kwa kuyasikiliza makundi mbalimbali yenye changamoto zinazokwaza ustawi wao wakati nchi ikianza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wao, Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), na Mhe. Laurent Deogratius Luswatula, wameshukuru kwa mapokezi makubwa waliyoyapata kutoka kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa Wizara na kuahidi kutoa ushirikiano na kuwa chachu ya mafanikio ya kuwaletea wananchi maendeleo kama walivyoaminiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Awali, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisema kuwa Wizara ya Fedha, ina wafanyakazi wachapakazi ambao wako tayari kuhakikisha kuwa kuna usimamizi mzuri wa uchumi na sekta ya fedha kwa ujumla kwa manufaa ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Ali Munde na Mhe. Laurent Deogratius Luswetula, waliapishwa jana na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kushika nyadhifa hizo, Ikulu-Chamwino, mkoani Dodoma.

Post A Comment: