Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya michezo nchini hatua inayosaidia kutoa ajira kwa vijana na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

 

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete Machi 7, 2022 katika ofisi za wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

 

“Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ni mdau muhimu katika kulea vipaji kwenye sekta ya michezo nchini, wamekuwa na ushirikiano mzuri na Serikali kwenye michezo hatua inayosaidia kutoa mchango wao kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika michezo mbalimbali” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

 

Aidha, Bw. Yakubu ameongeza kuwa zaidi ya michezo, chuo hicho kimebobea pia kufundisha lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili na Kichina na kuwaelekeza washirikiane na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili weweze kuwaandaa wataalamu wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ikizingatiwa jiji la Arusha ni kitovu cha wageni wengi wanaokuja nchini kwa kazi mbalimbali ikiwemo utalii.

 

“Hivi karibuni kutakuwa na kongamano la pili la kimataifa la idhaa zinazotangaza kwa lugha ya Kiswahili duniani ambapo mada mbalimbali zitatolewa na wabobezi wa Kiswahili, tumieni fursa hiyo muweze kuitangaza vizuri lugha yetu kimataifa” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete amesema chuo hicho kinatoa ufadhili kwa kuwalipia ada ya chuo wanafunzi wenye vipaji vya michezo chuoni hapo ambapo hadi sasa zaidi ya wanafunzi 26 wamenufaika na ufadhili huo.

 

“Chuo chetu kina idadi kubwa ya vijana wanaopenda michezo, tutaibua vipaji vingi katika taifa ili vijana waweze kujiajiri katika michezo kwa kuwa tunatambua usimamizi wa biashara kama biashara ikiwemo michezo” Dkt. Mwaitete.

 

Fauka ya hayo, Dkt. Mwaitete ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kupa pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) ambapo wanandelea kujenga miundombinu ya michezo chuoni hapo ili chuo hicho kiweze kuwa kituo bora cha michezo nchini na chuo hicho kinamatawi katika mikoa ya Manyara (Babati), Dodoma, Dar es salaam na Ruvuma (Songea).

 

Michezo inayofundishwa chuoni hapo ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, mpira wa netiboli pamoja na kutoa huduma za hosteli kwa timu za vijana za taifa zinapokuwa kwenye maandalizi mbalimbali ya michezo ya kimataifa.

 

Share To:

Post A Comment: