WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa sawa ya kufanya biashara katika mazingira bora na rafiki kwa biashara ili kukuza uchumi.


Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Machi 9, 2022) wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga Complex) lililoko barabara ya Bahi Mkoani Dodoma na kusema ameridhishwa na ujenzi wa soko hilo. 


"Lengo la maboresho haya kwa wafanyabiashara wadogo ni kutaka kutengeneza fursa zaidi  kwa kuwa na maeneo salama yanayotambulika na yanayoweza kutumika na taasisi za kifedha kutoa mikopo na fursa nyingine za kiuchumi."


Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa ubunifu na kuwataka viongozi hao waendelee kusimamia mradi huo na kuukamilisha kwa wakati pamoja na kubuni maeneo mengine ya nje ya mji Ili kukuza maeneo mengi zaidi kibiashara katika mkoa huo.


AIdha, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara wadogo wa mkoa huo wafuate utaratibu utakaowekwa na mkoa huo mara baada ya ujenzi kukamilika. "Serikali imeendelea kutafuta fursa za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo, hivyo jipangeni kutumia fursa hizo kwa uaminifu."


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema Mkoa wa Dodoma umefanya kazi kubwa ya kutekeleza mradi rafiki kwa wamachinga wa mkoa huo. “Niwasihi wakuu wa mikoa mingine kuiga mfano huu kwa kujenga miradi ya kuwapanga machinga kulingana na mazingira yaliyo katika mikoa yenu.”

Share To:

Post A Comment: