Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Tanzania inaendelea kunufaika pamoja na wananchi wake kwa kujenga uhusiano mzuri  na mataifa mbalimbali, zikiwemo nchi jirani zinazoizunguka.


Mhe. Mahundi amesema hayo wakati wa Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mawaziri, Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.

Amesema kupitia Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe kazi inafanyika kwa ushirikiano kuondosha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Tanzania na Malawi kupitia wataalamu wa rasilimali za maji, ikiwemo ujenzi wa mabwawa katika bonde hilo ambayo itakuwa suluhu ya mafuriko yanayoharibu mali mbalimbali ikiwamo mazao  kwa kujenga bwawa la Songwe Chini, na mazingira. Aidha, kuwezesha kilimo cha umwagiliaji zaidi ya hekta 6,000 na kupata nishati ya uhakika ya umeme kwa nchi mbili kugawana megawati zipatazo 180.

Mhe. Mahundi amesema hayo ni mafanikio ya mahusiano yaliyojengwa na viongozi wa nchi mbili katika kuhakikisha wananchi wanafanya kazi kwa maendeleo ya nchi zao. Amesema kazi hiyo ni matunda ya viongozi  Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mhe. Lazarus Chakwera , Rais wa Malawi.

Pamoja na hatua hiyo, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha huduma ya maji na miradi ya maji inakuwa endelevu na kutosheleza mahitaji ya jamii kwa sasa na vizazi vijavyo.

Kamisheni ya Bonde la mto Songwe inaundwa kwa Pamoja na nchi za Malawi na Tanzania, ambapo katika kikao hicho Mawaziri wamekubaliana na kusaini Kanuni za uendeshaji wa vikao vya Mawaziri.








Share To:

Post A Comment: