Na. Angela Msimbira TAMISEMI


Wanawake wa Mkoa wa Dodoma wafanya harambee  katika maadhimisho ya  Siku ya Wanawake  na kuchangia  kiasi cha shilingi milioni 17 kwa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam(JAI) wanaojishughukisha  na utoaji wa huduma za chakula kwa wagonjwa wasio na uwezo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.


Akiongoza harambee hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma  Mhe. Antony Mtaka  amesema, fedha taslim zilizopatikana ni kiasi cha shilingi milioni 6, ahadi milioni 11, taulo za kike pamoja na chakula.


Mhe. Mtaka amewataka wanawake wa Mkoa wa Dodoma kutumia maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka kusaidia vikundi vinavyojitoa kwa ajili ya kusaidia jamii ili vikundi hivyo viweze kusonga mbele katika suala zima la utoaji huduma ya kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii.


“Tuwekeze kwenye vikundi vyenye tija ambavyo vimejitoa kwa ajili ya kusaidia wananchi wetu ambao wanauhitaji, hawana uwezi na maskini kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiwekea hazina mbinguni, nawaagiza wanawake wote kufanya kitu cha tofauti katika maadhimisho yenu ya wanawake nchini” amesema Mtaka


Naye Mkuu wa Wilaya ya Chemba  Mhe.Simon Chacha amewasihi wanawake  kuwa na malezi mazuri  kwa  watoto wao bila  kuwaachia wasaidizi wa ndani pekee, kwa kuwa wanawake ndio walezi wakubwa ndani ya familia.


Akitoa risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Dodoma  Bi. Mary Barnabas ameishukuru Serikali  kwa kuwawezesha wanawake kupata mkopo  na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.


Aidha, maadhimisho ya sherehe ya wanawake kwa Mkoa wa Dodoma yalifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu “ Kizazi cha haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu  Tujitokeze kuhesabiwa”

Share To:

Post A Comment: