Na Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema wataendeleza ushirikiano na Wizara ya Kilimo ili kuhakikisha kuwa wanaimarisha Sekta ya Kilimo nchini.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa ameyasema hayo Februari 8,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe pamoja na wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara kujadili namna bora ya kuboresha kilimo.

Waziri Bashungwa amesema, "wakati sasa umefika wa kuhakikisha kuwa tunaunganisha mahitaji yetu na yale ya Wizara ya Kilimo kwa kuhakikisha kuwa bajeti inakua jumuishi na ya kutosha kutatua changamoto zinazokabili Sekta ya Kilimo kwenye Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa,"amesema.

Amesema, "hata ile mikopo yetu tunayoitoa kwenye halmashauri ya asilimia 10 iangalie namna ya kusaidia vikundi vya kilimo
vinavyolima kisasa kwa kuvipatia mikopo ili waweze kuboresha kilimo chao,"ameongeza Mheshimiwa Bashungwa.

Naye Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema wizara yake ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuhakikisha Sekta ya Kilimo inaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Hatuwezi kufanikiwa katika kilimo kama hatutashirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika mipango yetu ndio maana leo nimeona ni vyema kuja kukutana na wakuu wa mikoa moja kwa moja na vikao viendee hata kila baada ya miezi mitatu ili tuweze kupeana mrejesho na kupanga mipango ya baadae ya utekelezaji,"amesema Mheshimiwa Bashe.

Amesema, maeneo makubwa ambayo wataendelea kuyaangalia katika vikao hivi ni pamoja na huduma za ugani, kilimo na umwagiliaji na ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia mazao.

Pia amebainisha eneo lingine muhimu katika kuimairisha kilimo kuwa ni mfumo wa stakabadhi ghalani, upatikani wa mbolea ya uhakika kukomesha rumbesa katika uuzaji wa mazao kwa kuanzisha vituo vya masoko vijijini na kutoa miongozo inayosimamia uuzaji wa mazao ya wakulima.
Share To:

Post A Comment: