WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae semina kwa wabunge wote ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu yanayoendelea katika hifadhi ya Ngorongoro.

 

Mheshimiwa Majaliwa ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Februari 9, 2022) wakati alipochangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za kamati kwa mwaka 2021, Bungeni jijini Dodoma.

 

Waziri Mkuu amesema kuwa anaamini wapo wabunge wanaofahamu na wasiofahamau kuhusu yanaoendelea katika hifadhi hiyo “wakati tukiwa tunazungumza na wananchi, naiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya semina ya siku moja kwa wabunge wote ili wizara iwaambie kuna nini kule Ngorongoro, nini kilikuwepo awali na hali gani ipo sasa ili tuwe na uelewa wa pamoja”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa viongozi wa Serikali kukutana na wakazi wanaoshi katika eneo la hifadhi Ngorongoro na utekelezaji wake umeanza kwa kukutana na viongozi wa mkoa wa Arusha na Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

“Hatua iliyobaki ni kwenda Ngorongoro, nitafanya mikutano  eneo la Ngorongoro, nitafanya mikutano na wakazi wa eneo la Loliondo, baada ya kufanya haya yote itatusaidia kuendesha zoezi hili kwa amani kabisa kadiri itakavyokuwa imeamriwa”

 

Akizungumza wakati akichangia hoja ya kamati hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa Wizara italeta mabadiliko ya sheria ya hifadhi ya Ngorongoro kulingana na mapendekezo ya kamati na maoni ya wabunge.

 

“Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ya mwaka 1975 ni ya muda mrefu, mliyoongea Waheshimiwa wabunge yameonesha kuna mapengo kwenye sheria ile, msingi wa Sheria ile ni nguzo tatu za Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, inaonekana nguzo hizi zimeshindikana kushikiliwa kwa pamoja”

 

Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia inajali haki za binadamu “hatutafanya chochote ambacho kiko kinyume na haki za binadamu, na kwa kuwa tunaheshimu haki za binadamu hatutaingilia uhuru wa vyombo vya habari”.

Share To:

Post A Comment: