Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameiagiza Serikali kutoa maelekezo ya jumla juu ya uharibifu wa barabara Nchini kufuatia vilio mbalimbali vya Wananchi kuhusu adha wanayokumbana nayo. Dkt. Tulia ametoa agizo hilo leo Februari 9, 2022 wakati akiongoza kikao cha Bunge.


“Nilikuwa nimesema kuhusu habari ya TARURA, Serikali iseme jambo kwasababu tunapigiwa sana simu na Wananchi kuhusu changamoto ya barabara kukatika haswa katika kipindi hiki cha mvua, sasa toeni maelekezo ya jumla kwa TARURA nchi nzima ili barabara zinazosimamiwa na TARURA na hazipitiki wakazitazame ili Wananchi waweze kupata huduma”-Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson


Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde amesema >>”Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maelekezo yako uliyoyatoa kwetu na kwakuwa nimelipata suala hili vizuri. Nawaagiza Mameneja wote wa Mikoa wa TARURA pamoja na Halmashauri zote nchini kuanzia siku ya kesho waende wakafanye tathmini ya haraka iwezekanavyo na kutupatia Ofisi ya TAMISEMI ili tuweze kupeleka fedha za dharura kuhakikisha kazi inafanyika”


“Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kabisa kwamba hili agizo litatekelezeka na tutaleta taarifa ndani ya Bunge lako tukufu kabla ya Bunge hili kuisha”-Amesisitiza Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde

Share To:

Post A Comment: