WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote za mkoa wa Dodoma zianzishe vitalu vya kuzalisha miche ya zabibu ili kuwawezesha wakulima kupata mbegu kwa uhakika.

Pia, Waziri Mkuu amevitaka vyama vya ushirika wa kilimo cha zao la zabibu navyo vianzishe vitalu vya miche na kuwawezesha wanachama wake kupata mbegu bora kwa urahisi.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 06, 2021) alipozungumza na wadau wa uendelezaji wa zao la zabibu kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.”Tulime zabibu ya mvinyo na mezani.”

Waziri Mkuu ameziagiza taasisi nyingine, ikiwemo Jeshi la Kujenda Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza zianze kulima zao hilo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakulima wengine.

Amesema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo chake cha Makutupora iimarishe utafiti wa zao hilo ili kupata miche bora na yenye tija na kuifikisha kwa wakulima.

Amesema kupitia kampeni ya kuendeleza zao hilo, Serikali itasimamia kuhakikisha zabibu inayolimwa nchini inakuwa na ubora wa hali ya juu lengo likiwa ni kupata soko la uhakika.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kwa sasa Wizara ya Kilimo imeanza usajili wa wakulima wa zabibu ili waweze kuwatambua na kuwafikia kwa urahisi.

Amesema mbali na usajili wa wakulima, pia wizara hiyo imeanza majadiliano ya kuanzisha mfuko wa maendeleo ya zao hilo ambao utachangiwa na wenye viwanda na wakulima.

Kwa upande wake, Spika Job Ndugai amesema iwapo uwekezaji mkubwa katika viwanda vya kuchakata zao hilo kutakuwa na soko la uhakika na wengi watajitokeza kulima zabibu.

Pia, Spika ameuomba uongozi wa halmashauri ya jiji la Dodoma uruhusu watu kulima zabibu ndani ya jiji, pia ameshauri wananchi kulima zabibu katika maeneo ya makazi yao kama maua.

Naye, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthon Mavunde ameiomba Serikali iwasaidie wakulima katika kuboresha zao hilo kwa kuanza kuuza mchuzi wa zabibu badala ya kuuza matunda.

Wakulima wa zao hilo wameiomba Serikali iwasaidie katika upatikanaji wa pembejeo, mikopo pamoja elimu ya namna bora ya kulima zao hilo ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji wao.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Share To:

Post A Comment: