Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa jijini Dodoma.Miongoni mwa kazi kubwa za mkutano huo ni kumchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa.

CCM inamchagua Mwenyekiti wake mpya kufuatia kifo cha Dkt. John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 29,2021 kuhusu maandalizi ya mkutano huo katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema Wajumbe 1876 wa mkutano mkuu maalumu wa CCM wanatarajiwa kupiga kura jina moja litakalowasilishwa katika mkutano huo kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho .

Amesema mbali na wajumbe hao ambao watashiriki kupiga kura, wapo wageni 1,000 watakaoshiriki mkutano  wakiwamo kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini, wawakilishi wa vyama rafiki vilivyoshiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika na mabalozi.

Amebainisha kuwa  mkutano huo utaongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula na makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar,  Dk Ali Mohamed Shein.
Share To:

Post A Comment: