Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na uongozi wake unaowezesha Serikali kuendelea kuweka mazingira bora ya wananchi kupata huduma ya umeme na kutumia nishati hiyo kuchochea maendeleo.
Mhe. Homera amesema hayo leo, Oktoba 2, 2026, katika hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo imeshuhudiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini na unaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, pamoja na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Aidha Mhe. Homera amemshukuru na kumpongeza Makamu wa Rais kwa usimamizi wa karibu uliochangia kufikiwa kwa hatua hiyo, akisema mpango huo utawasaidia wananchi wanaohitaji kuunganishiwa umeme na wanakabiliwa na changamoto za kifedha.
Kupitia mpango huo, wananchi wa maeneo ya vijijini ambao awali walikuwa wakigharamia Shilingi 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme watawezeshwa kupata ufadhili wa gharama hiyo, huku wananchi wa maeneo ya mijini ambao gharama ya kuunganishiwa umeme ni Shilingi 320,000 wakipata fursa ya kugharamiwa kupitia mkopo wenye riba ya asilimia 10 kutoka CRDB.
Aidha, Waziri Homera ameipongeza Menejimenti ya Wizara ya Nishati, TANESCO, pamoja na Uongozi na Bodi ya Benki ya CRDB kwa ushirikiano uliowezesha maandalizi na utiaji saini wa mpango huo, akisema utakuwa na manufaa kwa wananchi, hususan wenye uwezo mdogo wa kifedha.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuibua mifumo bunifu ya kuongeza upatikanaji wa nishati na kuhakikisha umeme unatumika kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mhe. Homera ameahidi kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na ufanisi, ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika sekta ya nishati yanafikiwa na matokeo yake yanawanufaisha Watanzania wote.

Post A Comment: