Na Oscar Assenga, TANGA
MKUU mpya wa Wilaya ya Pangani, Mwanaidi Adadi Rajabu, ameahidi kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo pamoja na fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo.
Mwanaidi ametoa ahadi hiyo mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Pangani katika hafla iliyofanyika mkoani Tanga, akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuwapa nafasi za uongozi katika taifa.
Alisema wilaya ya Pangani ina fursa nyingi za maendeleo na uwekezaji ambazo zinahitaji kusimamiwa kwa karibu ili ziweze kuwanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
“Katika wilaya ya Pangani kuna fursa nyingi sana ambazo tunakwenda kuzisimamia, ikiwemo miradi ya Serikali iliyopo na ambayo itaendelea kuletwa katika wilaya yetu,” alisema.
Mwanaidi pia alitoa pongezi kwa Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuiunga mkono mkoa wa Tanga, hususan wilaya ya Pangani, kupitia miradi na uwekezaji mbalimbali wa maendeleo.
Alisema miongoni mwa fursa zilizopo Pangani ni Hifadhi ya Taifa ya Saadani, bahari, kilimo cha minazi pamoja na uwekezaji katika miundombinu, ikiwemo daraja kubwa linalojengwa kwa uwekezaji wa Serikali.
“Maendeleo ni mengi Pangani na fursa za uwekezaji ni nyingi. Tunamshukuru Rais kwa kuendelea kutuona wana-Pangani na kuendelea kuleta maendeleo katika eneo letu,” alisema.
Akizungumzia namna atakavyowatumikia wananchi, Mwanaidi alisema atahakikisha anakuwa karibu nao na kufuata nyayo alizotumia katika uongozi wake wa awali wilayani Korogwe, kwa kuwafikia wananchi walipo na kusikiliza kero zinazowakabili.
Alisema elimu ni miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele, akieleza kuwa tayari wamejipanga kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanaboreshwa, ikiwemo ujenzi wa madarasa na upatikanaji wa madawati.
Aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa wao ndio taifa la kesho, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika kuboresha elimu kwa ajili ya maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla.

Post A Comment: