Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameshuhudia uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB, ukiwa na lengo la kuongeza kasi ya wananchi kupata huduma ya umeme nchini.
Mhe. Ndejembi ameshuhudia uzinduzi wa mpango huo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, unaotekelezwa chini ya kaulimbiu “Kila Nyumba Itawaka – Tumekufikia, Tutakulipia na Utalipa Kidogo Kidogo,” akisema ushirikiano huo ni mfano wa namna Serikali na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali katika kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Kupitia mpango huo, wananchi wa maeneo ya vijijini watawezeshwa kuunganishiwa umeme kwa kupata ruzuku ya Shilingi 27,000 kwa kila kaya kutoka CRDB, ambayo si mkopo. Kwa upande wa wananchi wa maeneo ya mijini, watapata fursa ya kuunganishiwa umeme kwa mkopo kuanzia Shilingi 320,000 wenye riba nafuu.
Mhe. Ndejembi amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mission 300, inayolenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme barani Afrika, huku Tanzania ikiwa na lengo la kuwaunganisha watu milioni 8.5 na huduma ya umeme kati ya mwaka 2025 na 2030, sawa na kuwafikishia huduma hiyo takribani watu milioni 1.7 kwa mwaka.
“Miradi kama hii ni muhimu katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa ufanisi. Kupitia makubaliano haya, CRDB imejiwekea lengo la kufikisha huduma ya uunganishaji umeme kwa kaya 500,000 kwa mwaka,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa huduma hiyo, Mhe. Ndejembi amesema umeme ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na Taifa, akieleza kuwa mtoto anahitaji mwanga ili aweze kusoma, mkulima anahitaji umeme kuongeza thamani ya mazao yake, kijana anahitaji nishati kuwezesha ubunifu na teknolojia, huku mfanyabiashara akihitaji umeme kuongeza tija na kuchangia ukuaji wa uchumi.
“Hakuna Mtanzania anayepaswa kubaki nyuma kwa kukosa huduma ya msingi ya umeme,” amesema.
Aidha, Makamu wa Rais ameiagiza TANESCO kwa kushirikiana na CRDB kufanya tathmini ya matokeo ya mpango huo, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu gharama na masharti ya huduma hiyo, pamoja na kuhakikisha utekelezaji unaanza mara moja.
Mpango huo unatekelezwa chini ya kaulimbiu “Kila Nyumba Itawaka – Tumekufikia, Tutakulipia na Utalipa Kidogo Kidogo,” ikisisitiza dhamira ya kuwezesha wananchi kupata huduma ya umeme kwa urahisi na kwa masharti nafuu.










Post A Comment: