Na Denis Chambi, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani amewapa siku 30 wakuu wa Wilaya zote 9 kuhakikisha kuwa wanatumia muda huo kuwaelimisha wananchi kuanzia ngazi ya Kijiji, kata na wilaya juu ya mpango wa Serikali kuelekea dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Dkt.Batilda ametoa agizo hilo Leo October 2, 2026 wakati akiwaapisha wakuu wa Wilaya za Tanga Pangani na Korogwe pamoja na kula viapo vya utii kwa wateule wa Rais walioteuliwa hivi karibuni ambao ni pamoja na wakurugemzi wa Halmashauri pamoja na makatibu tawala ambapo pia amewasisitiza kila mmoja ahakikishe katika eneo lake analosimamia na kuongoza anaimarisha suala la ulinzi na usalama.
"Dira ya 2025 ndio msingi wa nchi yetu kufikia 2050 hivyo Kila Mkuu wa Wilaya ahakikishe anaandaa mpangokazi wa kwenda kujipanga na kuelezea jinsi gani utekelezaji wa dira utafanyika hatutaki tuone dira inabaki kwenye madawati lazima wananchi wako waelewe dira inasema na inataka nini kitaifa na hivyo Kila Mkuu wa Wilaya ahakikishe anaandaa mpango kazi wa dira katika ngazi ya kata Kijiji ndani ya siku 30" amesema Dkt Buriani.
Aidha amewataka wakuuu wote wa Wilaya 9 za mkoa huo kwenda kusimamia na kuimarisha maeneo yote ambayo ni vyanzo vikuu vya uchumi pamoja na kuzisimamia Halmashauri katika suala la ukusanyaji wa mapato kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema kuwa asilimia 40 ya mapato yanayokusanywa ndani ya mkoa wa Tanga yanapatikana ndani ya jiji la Tanga hivyo kumtaka mkuu wa Wilaya hiyo Edwin Mathew kuangalia kwa ukaribu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ambayo ni pamoja na ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi linalotoka Uganda hadi Chongoleani, mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta , upanuzi wa Uwanja wa Ndege, mradi wa Hatifungani unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Tanga Uwasa pamoja na mingine.
Aidha katika kuweka mazingira safi na salama mkuu huyo wa mkoa ametangaza kuwa kila jumamosi ya kwanza ya mwezi itakuwa ni siku maalum kwaajili ya usafi ambapo wananchi wote watapaswa kushiriki kwenye maeneo yao.
"Kila jumamosi ya kwanza ya mwezi tutakuwa na msalagambo tutashirikiana na wananchi kwa pamoja kufanya usafi maduka yatafunguliwa saa 3 asubuhi, lakini tumeunda kikosi kazi cha vijana 50 ambao watakuwa wanapita kila mtaa kuleta taarifa za maeneo ya uchafuzi watakaofanya makosa ya utupaji taka ovyo kuna faini ambayo imeshabainishwa" amesisitiza Dkt. Buriani.
Akizungumzia suala la elimu kuelekea 2027/2028 ambapo wanafunzi wa darasa la sita na la saba wataanza kidato Cha kwanza Dkt Buriani amewataka wakuu wa Wilaya wote kuandaa taarifa za hali ya upungufu wa madawati na madarasa na kutatuta namna ya kuweza kukabiliana na changamoto hiyo kabla mwaka mpya wa masomo haujaanza.
"Ifikapo 2027-2028 watoto wa darasa la saba na la sita kwa pamoja wanakwenda kuanza kidato cha kwanza nataka nipate taarifa kutoka katika Kila wilaya kila mwisho wa mwezi tuna upungufu wa madawati kiasi gani ni lazima mkuu wa Wilaya ujue tutaingiza watoto wangapi tuna madarasa mangapi na tumejipanga vipi" amesisitiza Dkt Buriani.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa ameawagiza wakuu wote wa Wilaya kuhakikisha wanatenga hakta 1000 kwaajili ya uwekezaji pamoja na kuyalinda maeneo yote ambayo yaliyotengwa yasitumike kwa shughuli nyingine ikiwemo wananchi kuyatumia kwaajili ya makazi na kilimo.



Post A Comment: