Na Denis Chambi, Tanga.
SERIKALI ya Mkoa wa Tanga imeunda kikosi kazi maalumu kitakachokuwa kinatoa elimu kwa wananchi pamoja na kuhamasisha juu ya utunzaji wa Mazingira kuanzia ngazi ya mitaa na vijiji pamoja na kukamata wale wote watakaobainika kutupa taka ovyo ambao watakabiliwa na faini ya kuanzia Shilingi 50,000.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Tanga Mustafa Seleboss akishiriki na wananchi katika zoezi la Msalagambo huo uliopewa jina la Balozi Dkt Batilda Mazingira Day ambalo litafanyika Kila jumamosi ya kwanza ya mwezi.
Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani akiwa pamoja na wananchi na baadhi ya Askari wa vyombo vya ulinzi na usalama walioshiriki katika Msalagambo huo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani wakati akizindua Msalagambo maalumu wa Kila mwezi ambapo amesema kuwa kikosi hicho cha vijana Hamsini pamoja na kutatekeleza sheria ndogo za mazingira zilizopo chini ya Halmashauri watakusanya taarifa kubaini sehemu zote ambazo zitahitajika kufanyiwa usafi kisha kuzipeleka kwenye Halmashauri kwaajili ya kupeleka gari la kuzolea taka.
"Tutakuwa na kamati ya ukaguzi itakayohusika na kubaini changamoto, kutoa elimu na maelekezo yatatolewa na pale sheria itakapokiukwa na mhusika akaonekana anaendelea kukaidi hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa miongozo baadaye tusije tukalaumiana na faini imeandikwa kwenye sheria ndogo ya mazingira na Halmashauri faini ya chini kabisa ni elfu hamsini" amesema Dkt Buriani.
Adha ameongeza kuwa kikosi hicho kimekaguliwa na kinatabuliwa rasmi na Baraza la mazingira la Taifa (NEMC) ambao watawapa ithibati kwa kushirikiana na Halmashauri ya jiji la Tanga tayari kuwapa ruksa ya kukabiliana na watakaokiuka sheria za mazingira zilizopo na hukumu zitatolewa papo kwa papo huku faini zitakazokusanywa zikiingizwa kwenye mfumo rasmi wa ukusanyaji mapato.
"Timu hii haitakuwa juu ya sheria, watakula kiapo hawatopokea rushwa wala kutumia nguvu kukamata na tozo zote zitakazokusanywa kisheria kupitia Pos-Mashine na risiti zitatolewa, tunataka kuhakikisha kwamba kosa linathibitishwa na hatua zitachukuliwa hatukusudii kutoza faini kwa wananchi tunakusudia kuboresha mazingira yetu" amesisitiza.
Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Msaragambo huo katika stendi ya Daladala barabara ya 12 jijini Tanga kuhamasisha zoezi la kuweka mazingira katika hali ya usafi na salama.
Amezitaka Halmashauri zote 11 zilizopo ndani ya mkoa huo chini wa wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa wanatekeleza Msaragambo huo ambao umepewa jina la Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day ikiwa na kauli mbiu maalumu ya utunzaji mazingira huku akiwataka wananchi kushiriki zoezi hilo kwa hiari.
Amebainisha kuwa Mkoa wa Tanga katika pato la Taifa unachangia kiasi cha Shilingi Bilioni 6 kwa mwezi ukiwa unashika nafasi ya 6 katika Mikoa yote hapa nchini akisisitiza kuwa mafanikio hayo yaendane sambamba na kuweka mazingira safi kuanzia ngazi ya kaya.
Akimwakilisha Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini, Meneja wa Baraza hilo Kanda ya Bagamoyo Ndimbumi Mboneke amebainisha kuwa kisheria kila mwananchi anawajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama wakati wote pamoja na kutoa taarifa za uharibifu wa mazingira katika Mamlaka husika.
Aidha Baraza hilo limekabidhi cheti maalum cha shukrani kwa Mwananchi wa mkoa wa Tanga Mohamed Hilal kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya utunzaji wa mazingira likitaka kila mtanzania kuiga mfano huo.
"Sheria ya mazingira imetoa haki kwa kila Mtanzania kuishi katika mazingira safi na salama lakini pia imetoa wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi na salama na imempa wajibu wa kutoa taarifa anapoona kuna uharibifu wowote hivyo tunatoa wito kwa kila mmoja kuiga mfano huu"amesema Mboneke.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Tanga Mustafa Seleboss ameeleza utayari wao wa kupokea na kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa huo akianza kuwaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Machinga waliopanga biashara zao katikati ya stendi ya Daladala.
"Hili zoezi tumelipokea wananchi wa jiji la Tanga na yale yote uliyoelekeza kwetu sisi ni amri sio ombi, jina lako tutalienzi kila ilifika tarehe moja ya mwezi tutafanya usafi maalum na kuanzia sasa tutavunja vibanda vyote ambapo ukifika kumejaa uchafu mwingi tutatoa mawe yote yaliyopo hapa stendi ambayo wanayatumia kuwekea mizigo yao" amesema Seleboss.







Post A Comment: