Na Denis Chambi Tanga.

WAKATI Serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kutoa elimu kwa wananchi juu ya Mvua za El-Nino Wakala wa maji  na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga imesema kuwa imejipanga kuhakikisha miradi yote iliyopo mkoani humo inayotoa huduma kwa wananchi haiathiriki ikiwa ni kutekeleza maagizo waliyopewa.

Haya yameelezwa na  Meneja wa  Wakala  wa maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mhandisi Alkam Sabuni wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea hali ya utoaji huduma kwa wananchi ambapo amesema kuwa wamechukua hatua kuu tatu ambazo ni pamoja na kuzungushia ukuta katika visima ili kukinga mafuriko yasiweze kuchafua ubora wa maji au kuharibu miundombinu iliyotengenezwa. 

"Sisi kama sekta ya maji mkoa wa Tanga tumejiandaa vyema kupunguza madhara yanayoweza kutokana na mvua za El-Nino na tumejiandaa katika namna kuu tatu kwanza kwenye usanifu wa miradi yetu katika  maeneo  ambayo tunatumia  maji yaliyopo chini na ya rdhi miundombinu  yetu yote ya visima virefu tumezungushia kuta ili kuzuia mafuriko yasichafue ubora na usafi wa maji yanayotumiwa na wananchi" amesema Sabuni 

"Eneo lingine ni kwenye madawa ya kutibu maji katika yale maeneo ambayo tunadhani kutakuwa na ongezeko la tope katika maji  tumejipanga vizuri na tuna madawa ya kutosha kuweza kutibu maji, tumetoa pia taarifa kwa wateja wetu kuwataka wahifadhi maji ya kutosha majumbani ili ikitokea kama athari zimekuwa kubwa wawe na maji ya kutosha na katika yale maeneo ambayo kuna uwezekano mkubwa wananchi wanaweza kuondoka kwenye maeneo hayo tunaendelea kufanya tathmini" ameongeza Meneja huyo.

Aidha amewataka wananchi kuwa wazalendo  kulinda na kutunza miundombinu ya maji iliyopo ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele kukemea uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kukata miti ovyo hali ambayo inaweza kusababisha ukosefu wa huduma ya maji na kuathiri vyanzo vilivyopo.

"Niwaase sana wananchi wawe wazalendo  wafahamu kwamba maji ni usalama wa nchi pale ambapo wanaharibu miundombinu na kuchafua maji tayari wanatishia usalama wa nchi na wanaisababishia Serikali hasara ya kutibu maji na wananchi ,  tunatumia gharama kubwa kujenga miundombinu iliyopo hivyo ni lazima ilindwe" amesisitiza Sabuni.

Meneja huyo ameongeza kuwa mkoani Tanga sasa ipo miradi mbalimbali inatekelezwa  ambayo inalenga kuboresha hali ya utoaji huduma na upatikanaji wa maji kwa wananchi ambapo jumla ya miradi 79 ikigharimu kiasi cha Shilingi Milioni 104 ambapo ipo katika hatua za utekelezaji ikitarajiwa kukamilika ifikapo  June 2027. 


Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mhandisi Alkam Sabuni akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilda Buriani wakati alipofika ofisini kujitambulisha.Picha na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini 'RUWASA' Mkoa wa Tanga kwa sasa inahudumia watu zaidi ya Milion 2,400,000 , zaidi ya kaya 635,514 ambapo mpaka sasa katika hali ya utoaji wa huduma ya maji wamefikia asilimia 75 wakitarajia kufikia asilimia 85 baada ya kukamilika kwa miradi inayoendelea kitekelezwa.

Sabuni ameongeza kuwa mpaka sasa mkoani Tanga kuna vyombo (Sibiuso) 42 vilivyosanilowa kisheria chini wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) ikiwa lengo lao ni kuhakikisha miradi yote iliyopo katika maeneo ya wananchi inalindwa na kuendelea kutoa huduma iliyokusudiwa na Serikali.
Share To:

Post A Comment: