Na Denis Chambi, Tanga.


WAKATI Serikali na wadau mbalimbali wakiendelea kuweka mipango madhubuti ambayo ni tahadhari juu ya ujio wa Mvua za El- Nino Mamlaka ya Bima Tanzania 'TIRA' imesema kuwa inaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa bahari wakiwemo wavuvi wanaofanya shughuli zao za usafirishaji wa abiria na mizigo ili wawe na huduma ya bima itakayowasaidia pindi watakapopata changamoto.


Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini Dk. Emmanuel Lupilya wakati alipokuwa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa ujezi na uchukuzi David Kihenzile alipotembelea na kukagua Banda la Mamlaka hiyo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya usafirishaji na usafiri majini Duniani iliyofanyika mkoani Tanga  wakieleza namna jinsi walivyojipanga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa bahari.


Dk. Lupilya amesema kuwa lengo lao ni kuhakikisha  kuwa mizigo yote ya ndani na nje ya nchi  inayosafirishwa kupitia usafiri wa majini katika vyombo mbalimbali ikiwemo Mashua viwe vimekatiwa bima ambayo itakuwa ni kinga itakayowasaidia pindi yanapotokea majanga.


"Tunaendelea kutoa elimu kwa watu wenye Mashua wanaosafirisha mali, mizigo na abiria lakini pia wameweza katika vyombo vyao ni lazima tutengeneze bidhaa muhimu inayomlinda Mmiliki huyu, tumejipanga kuhakikisha kwamba mizigo yote inayoingia iwe ya Tanzania au nje ya nchi na yenyewe ni lazima ikatiwe bima tutawaelimisha ili kukinga athari zinazoweza kujitokeza wakati wakifanya shughuli zao hili ni eneo ambalo tunakwenda kuliwekea msisitizo" amesema


Aidha Meneja huyo ameipongeza Serikali kwa jinsi inayoendelea kuboresha miundombinu ya bahari pamoja na Bandari ikiwemo Bandari ya Tanga ambayo imeanza kuleta manufaa akisema kuwa maendeleo hayo yaendane na mabadiliko kwa jamii kupitia fursa zilizopo kwenye uchumi wa buluu .


Ameongeza kuwa TIRA imemfanya mazungumzo na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kushirikiana kwa lengo kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya usafiri vinavyoingia hapa nchini viwe vimekatiwa bima hii ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya bima.


"Tayari tumefanya majadiliano na wenzetu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)  kuhakikisha kuwa wale wanaoingia  na vyombo vyao lazima vikatiwe bima hapa nchini lakini pia shughuli zote zinazofanyika za kuingiza na kutoa  mizigo ni lazima vikatiwe bima hii ni kwa mujibi wa Sheria ya bima namba 394 lakini pia tunasisitiza ulinzi wa mali zao" amesema Meneja huyo.


Akifunga maonesho hayo kitaifa kwa mwaka 2026 Naibu Waziri wa ujezi na uchukuzi David Kihenzile amesema kuwa sekta ya usafiri majini umekuwa ni kiungo muhimu kwa Tanzania na mataifa mengine ambapo zaidi ya nchi saba zinategemea na kuchukua   mizigo mbalimbali  kutoka hapa nchini.


Ameongeza kuwa  kulingana na takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania 'TRA' sekta ya usafiri na usafirishaji majini umekuwa ukichangia asilimia 40 ya Pato la Taifa.


"Sekta hii ni muhimu kwa Taifa letu na Duniani kote, nchi yetu inahudumia  zaidi ya nchi saba zikitegemea  mizigo kutoka Tanzania , kulingana na taarifa za  mapato ya TRA  asilimia 40  ya pato la  Taifa inachangiwa  na  usafirishaji wa majini hivyo sekta hii ni muhimu sana kiuchumi inatusaidia sana" amesema Naibu Waziri .


Hata hivyo ameiagiza Wakala wa  Meli Tanzania TASAC kwa kushirikiana na  ZMA  kuhakikisha zinaendelea kufanyanga ukaguzi wa mara kwa mara  kwenye vyombo vyote vinavyotumia usafiri huo ili kuepukana na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza wawapo safarini.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: