Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) umeendelea kuimarisha juhudi za kuweka msingi wa utekelezaji endelevu wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, kwa kuwashirikisha wadau muhimu katika ngazi ya shule na jamii Mkoani Arusha.

Hatua hiyo imefanyika kupitia kikao kilichowakutanisha Kamati za Lishe za Shule za Msingi Kioga na Ilkisongo, zilizopo Kijiji cha Oloigeruno, Kata ya Ilkidinga, Mkoani Arusha, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha ushiriki wa wadau katika utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni.

Akifungua kikao hicho Septemba 24, 2026, Afisa Mifugo wa Mkoa wa Arusha, Bi. Winfrida Joseph, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha jitihada za kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni zinakuwa sehemu ya mfumo endelevu unaoshirikisha shule, wazazi, jamii, wazalishaji na wadau wengine wa Tasnia ya Maziwa.

Kwa upande wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Afisa Masoko Mwandamizi, Bw. Hamis Kiimbi, amesema ushiriki wa Kamati za Lishe ni muhimu katika kuhamasisha wanafunzi, walimu na wazazi kutambua umuhimu wa maziwa katika lishe, afya na ustawi wa watoto, huku akieleza umuhimu wa kuweka mazingira yatakayowezesha mpango huo kutekelezwa kwa ufanisi katika ngazi ya shule.

Amesema utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali, shule, wazazi, wazalishaji na wasindikaji wa maziwa, ili kuhakikisha upatikanaji wa maziwa salama na yenye ubora unakuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.

Akizungumza kwa niaba ya C-SDTP, Mratibu wa Mradi kutoka Wilaya ya Arusha DC, Bw. John Matemu, amesema mradi unaendelea kushirikiana na wadau katika kujenga uelewa na kuweka misingi ya utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, sambamba na kuimarisha mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Maziwa.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati za Lishe, Bw. Emanuel Isaya, amesema kikao hicho kimewapa fursa ya kujadili kwa pamoja fursa na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, pamoja na namna kila mdau anavyoweza kutekeleza wajibu wake.

Aidha, kikao hicho kilishirikisha wadau kutoka sekta binafsi, akiwemo Bi. Jackline Ngasa, Msindikaji wa Maziwa kutoka Asili Dairy, ambaye alishiriki katika majadiliano yaliyolenga kuimarisha uhusiano kati ya shule na wadau wa Tasnia ya Maziwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa salama na yenye ubora.

Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi na juhudi zinazoendelea Mkoani Arusha za kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni, kwa kuimarisha ushirikiano wa wadau kuanzia ngazi ya shule, jamii hadi wadau wa Tasnia ya Maziwa.

Kupitia ushirikiano huo, TDB na C-SDTP zinaendelea kuhamasisha wadau kutambua nafasi yao katika kuhakikisha unywaji wa maziwa shuleni unakuwa sehemu ya juhudi za kuboresha lishe na ustawi wa wanafunzi, huku ukiendelea kufungua fursa za soko kwa wazalishaji na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa maziwa.

Juhudi hizi pia zinaendana na maandalizi ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni 2026, inayotarajiwa kufanyika tarehe 30 Septemba 2026 Mkoani Arusha, ikiwa na kaulimbiu “Nyumbani, Shuleni Maziwa kwa Lishe Bora.”
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: