Articles by "TANROADS"
Showing posts with label TANROADS. Show all posts

Serikali imesema inalipa kipaumbele cha juu malipo kwa makandarasi wa ndani kama mkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa na kuendeleza uwezo wa kitaalamu wa wazawa katika sekta ya ujenzi.

Akizungumza Jumapili Juni 8, 2025 mkoani Mwanza katika mjadala na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema tayari zaidi ya Shilingi bilioni 90 zimeshalipwa kwa makandarasi wa ndani kati ya deni la zaidi ya bilioni 260, lengo likiwa ni kuhakikisha fedha za miradi ya ujenzi zinazunguka ndani ya nchi.

“Makandarasi wetu wa ndani wakilipwa, uchumi wa nchi unaimarika kwa sababu hela inabaki ndani yetu wenyewe. Rais Samia amenipa maagizo rasmi kuwa kipaumbele cha kwanza kiwe kwa malipo ya makandarasi wetu wa ndani,” amesema Ulega.

Ameeleza kuwa katika muda mfupi tangu kuteuliwa kwake kuongoza Wizara hiyo, tayari wamelipa kiasi hicho kwa utaratibu wa awamu huku takriban Shilingi bilioni 186 zikiwa bado hazijalipwa. Hata hivyo, ametoa hakikisho kuwa serikali itaendelea kulipa madeni hayo hatua kwa hatua kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha.

“Fedha zikipatikana hata kama ni kidogo, cha kwanza ni kuwalipa makandarasi wa ndani. Tunafanya hivi kwa nia ya kulinda uchumi wetu, kuzuia kufilisika kwa makandarasi wetu, na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” amesisitiza.

Waziri huyo amebainisha kuwa, pamoja na changamoto ya madeni mapya kutokana na kazi zinazofanyika kila siku, serikali inajitahidi kuwa na mfumo thabiti wa kulipa madeni hayo bila kuathiri utekelezaji wa miradi mipya.

Kuhusu suala la kutumia wataalamu wa ndani, Ulega amesema serikali inafanya mabadiliko makubwa kuhakikisha wataalamu na kampuni za ndani yananufaika moja kwa moja na miradi ya ujenzi. Amesema mabadiliko haya ni maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa Rais Samia ambaye amedhamiria kuhakikisha wazawa wanajengewa uwezo wa kufanya kazi kubwa kama za kimataifa.

Akitolea mfano, Waziri Ulega alisema mwaka 2023 wakati wa maafa ya mvua za El Niรฑo na Kimbunga Hidaya, Rais Samia alitoa kibali cha Shilingi bilioni 562 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu iliyoharibika, ambapo zaidi ya bilioni 400 kati ya hizo zilipelekwa kwa makandarasi wa ndani kupitia mikataba 72 kati ya 82.

Vilevile, ameeleza kuwa serikali imefanya mabadiliko ya kanuni za ujenzi ambapo sasa miradi yote yenye thamani ya chini ya Shilingi bilioni 50 inapaswa kufanywa na makandarasi wa ndani pekee, huku miradi ya zaidi ya kiwango hicho ikigombewa na wageni kwa masharti ya kushirikisha makandarasi wa ndani.

“Sasa hivi wageni hawaruhusiwi kugombea kazi za chini ya bilioni 50. Aidha, tunatengeneza kanuni mpya zitakazowalazimisha wakandarasi wa nje kushirikiana na wa ndani katika kila mradi,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, serikali inatarajia kuona mabadiliko haya yakileta matokeo chanya ya muda mrefu katika kukuza uwezo wa makandarasi wa ndani kiufundi, kifedha na kiteknolojia.

"Matumizi mengine ikiwa ni ya utalii na watani zangu wasukuma wanaweza kutaka kuja kufanya harusi zao, kurekodi kwaya, kaswida na mambo mengine ya kijamii, kimsingi sisi tumekasimiwa mamlaka na Mhe. Rais kwahiyo mimi ninayo kazi ya kumuomba kwamba yeye na kumjulisha kwamba wapo watanzania wanaotaka kuja kufanya kwaya, kurekodi kuja kufanya mpaka picha za harusi hapa.

Kabla ya kutoa vibali, tutamshirikisha Mhe. Rais na niwahakikishie tukipewa kibali sisi maana yake tutatumia njia ya kuwaambia watanzania wote kuhusu utaratibu maalum kwaajili ya usalama wa watu, watumiaji hao kwasababu hapa malori yatakuwa yanapita tena kwa kasi.

Tumeshaanza kupokea maoni mfano kutoka kwa baadhi ya wabunge wanasema wananchi wasilipishwe lakini malori ya biashara lazima yachangie kwasababu hapa panahitajika hapa maintanance lakini jambo hili halijafika mwisho, linahitaji mjadala na linahitaji kuridhiwa na litakaporidhiwa tutatangaza hadharani."- Mhe. Abdallah Ulega Waziri wa Ujenzi wakati wa mjadala wa #MamaNiMjenzi leo Juni 08, 2025, Jijini Mwanza kwenye daraja la Kigongo-Busisi.

 


Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuanza kutumika kwa daraja la Kigongo- Busisi kunatarajiwa kuimarisha na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji ndani na nje ya nchi na kuondoa changamoto ya upotevu mkubwa wa muda uliokuwepo awali kutokana na miundombinu iliyokuwepo.

"Hili daraja ni njia fupi ya kumfikisha mtu Bukoba mkoani Kagera leoleo kwa wakati muafaka, wakati zamani mtu akitaka kwenda Bukoba kabla ya maendeleo makubwa ya barabara katika nchi yetu hayajafika alikuwa lazima aende mpaka Kenya na Uganda kisha uingie Tanzania. Kwenda Bukoba ilikuwa lazima uende nchi mbili za jirani, tumeondoa unyonge huo." Ameeleza Waziri Ulega.

Leo Jumapili Juni 08, 2025 katika mjadala wa #MamaNiMjenzi, wenye lengo la kuangazia mafanikio ya miaka minne ya sekta ya Ujenzi nchini, Waziri Ulega ameeleza kuwa daraja hilo pia litaunganisha mikoa ya Mwanza, Geita, Kigoma, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Burundi, akisema Daraja hilo ni miongoni mwa viungo vitakavyokuza utengamano wa Afrika ya Mashariki.

Katika Mjadala huo ulioongozwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, Waziri Ulega amebainisha kuwa kutokana na daraja hilo kuwa na sifa za Daraja la Kitaifa, wamewaalika pia Mabalozi kutoka nchi jirani ili kuweza kushiriki katika uzinduzi wa daraja hilo baadae mwezi huu.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Daraja la Kigongo–Busisi ni sehemu muhimu ya kuunganisha miundombinu ya kimkakati inayowezesha usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR na barabara za mikoa, na hivyo kuongeza tija ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu nchini.

Akizungumza katika mjadala maalumu siku ya Jumapili Juni 8, 2025 mkoani Mwanza kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya ujenzi, Waziri Ulega amesema hatua hiyo ni sehemu ya mipango ya serikali kufungamanisha miradi ya barabara, reli na bandari ili kuongeza ufanisi wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.

“Uwezo wa daraja hili ni wa kipekee katika kuunganisha miundombinu ya SGR ambayo inabeba mzigo mkubwa sana. Kipande cha Mwanza hadi Isaka kimeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 50,” amesema Waziri Ulega.

Amefafanua kuwa reli hiyo itaunganishwa kutoka Mwanza hadi Tabora, Tabora hadi Dodoma, na kuendelea hadi Kigoma na Msongati, hivyo kuwezesha mtiririko wa usafirishaji wa mizigo kutoka na kwenda kwenye maeneo mbalimbali ya nchi na ukanda wa Maziwa Makuu.

Akizungumzia barabara za kuunganisha daraja hilo, Waziri Ulega amesema tayari serikali imeshampata mkandarasi wa kujenga barabara ya Mwanza hadi Usagara, na kwa sasa wapo kwenye mazungumzo ya kushusha gharama za mradi huo ili kusaini mkataba.

“Nina matumaini makubwa kwamba kabla ya siku ya uzinduzi wa Daraja hili, ambayo itaongozwa na Rais Samia, tutakuwa tumesaini mkataba wa barabara ya Mwanza–Usagara, na mkandarasi ataanza kazi mara moja ili aunganishe na miundombinu ya SGR,” ameeleza.

Mbali na hilo, serikali inajiandaa pia kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema–Nyahunge kabla ya Juni 19, 2025 (tarehe ya uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigongo–Busisi) ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari na kuweka njia mbadala ya kuunga mkono matumizi ya Daraja la Kigongo–Busisi.

Daraja hilo la kimkakati limetajwa kugharimu takriban Shilingi bilioni 716, ikiwa ni fedha zote kutoka kwenye kodi za Watanzania kwa asilimia 100, ikijumuisha pia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

 


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Kikombo – Chololo - Mapinduzi inayokwenda kwenye Makao Makuu mapya ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kukamilisha kazi hiyo ifikapo Desemba mwaka huu.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 16.4 kwa kiwango cha lami umekuwa ukisuasua kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni upungufu wa wafanyakazi na mitambo ya ujenzi. 

Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo akiwa amefuatana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax pamoja na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman na watendaji wengine wa wizara yake.

“Tumekagua barabara hii na sijaridhishwa na kasi ya utekelezaji wake. Natoa  maelekezo mahususi kwa barabara hii, mkandarasi afanye kazi usiku na mchana, aongeze vifaa na mitambo ya ujenzi lakini pia azalishe ajira kwa wakazi wa maeneo haya ili barabara hii ikamilike kwa viwango na muda tuliompa kimkataba”, amesema Ulega.

Waziri Ulega amemuagiza mkandarasi ambaye ni kampuni ya CHICO kuhakikisha anaboresha mpango kazi wake ili aweze kukamilisha kazi zilizobakia zikiwemo ujenzi wa makalvati pamoja na madaraja katika barabara hiyo.

Aidha, Waziri Ulega amebainisha kuwa Serikali hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji la Dodoma.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax ameeleza kuwa ni matumaini yake ujenzi wa barabara hiyo utakamilika kwa muda uliopangwa na ikiwa na ubora na viwango vinavyotakiwa.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj. Jabir Shekimweri amewashukuru Mawaziri hao kwa kufika na kukagua hatua za barabara hiyo  kwani lengo la barabara hiyo ni kuleta muunganiko na ukaribu kati ya Wilaya za Dodoma Mjini na Chamwino hivyo utachochea maendeleo katika maeneo husika.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko amewahakikishia mawaziri hao kuusimamia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ili ikamilike kwa muda uliopangwa ambapo hadi sasa umefikia asilimia 51.






WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itatumia kiasi cha shilingi bilioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuboresha usafiri na kuifungua mikoa hiyo kiuchumi.

Akizungumza mkoani Mtwara, Ulega alisema barabara na madaraja hayo yatajengwa kupitia barabara za Mtwara –Mingoyo (Mnazi mmoja)-Masasi  itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 401 huku barabara nyingine ya Mtwara Tandahimba-Newala-Masasi itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 268 hadi kukamilika kwake.

Waziri Ulega amewaambia wananchi wa Mtwara kwamba kiasi hicho kikubwa cha fedha katika ujenzi wa miundombinu hiyo unaonyesha dhamira ya dhati aliyonayo Rais Samia kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na lengo kubwa ni kuhakikisha inafunguka kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kiuchumi.

“Wananchi wa mikoa ya Kusini, ninawaletea salamu hizi za Rais wenu Samia Suluhu Hassan. Hizi barabara zikikamilika kutakuwa na taa za barabarani takribani 4800 kutoka Mtwara hadi Masasi. Kusini kutang’ara kwa mwanga nyakati za usiku na kutapendeza. Kwenye barabara nzuri, uchumi unafunguka na kwenye mwanga kwa saa 24, biashara zinafanyika muda wote,”alisema Ulega.

Ulega yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambako pamoja na mambo mengine anafuatilia maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuangalia maendeleo ya ukarabati wa barabara na miundombinu mingine ya ujenzi iliyoharibiwa wakati wa mvua za masika na kimbunga cha Hidaya kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu.

Akitoa mchanganuo, Ulega alisema katika kiasi hicho cha fedha, zaidi ya shilingi bilioni 230 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti (m 84) ili kuzifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi kupitia usafirishaji wa abiria na mazao.

 “Kazi kubwa inafanywa katika mikoa ya Kusini na ni dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuufungua Mkoa wa Mtwara ili mazao ya biashara na chakula yapate thamani kwa kufika katika masoko kwa urahisi pamoja na kupunguza gharama  na muda wa usafiri”, amesisitiza Ulega.

Kuhusu faida nyingine za miradi hiyo ya ujenzi, Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga aliwaambia wananchi wa mikoa ya Kusini kwamba wakandarasi waliopewa zabuni ya kujenga barabara hiyo watatakiwa pia kutia huduma nyingine kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho, nyumba za madaktari na mambo mengine kwa mujibu wa mkataba.

Ulega amewataka wakandarasi wanaojenga barabara ya Mnivata-Masasi kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wazawa wa maeneo barabara inakopita kwa kushirikisha ofisi za Serikali za Mtaa na Kata za Wilaya.

Amesisitiza kuwa licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara, miradi hiyo inapaswa kuzalisha ajira kwa wananchi wazawa na kuacha ujuzi ili uweze kuwasaidia katika majukumu mengine ya kijamii na kiuchumi.

Ulega ameitaka TANROADS kukamilisha taratibu za kuwapata wakandarasi watakaotekeleza miradi Jumuishi ya kijamii (CSR) ili ujenzi wa barabara uende sambamba na miradi hiyo ambayo itahusisha ujenzi wa Kituo cha Mabasi, ghala, ununuzi  wa mashine za kubangulia  korosho, mabweni ya shule, ununuzi wa X-Ray na gari la wagonjwa.

Ulega ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia ameshatoa kibali cha ukarabati wa barabara ya Mtwara hadi Mingoyo (Mnazi Mmoja) na Mingoyo hadi Masasi ambapo takribani Bilioni 152 zitatumika katika barabara hiyo.

Naye, Meneja wa TANROADS,  Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John ameeleza mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi China WuYi umegawanywa katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ya Mnivata - Mitesa (km 100) unatekelezwa kwa muda wa miezi 36 na sehemu ya pili ya Mitesa - Masasi (km 60) na ujenzi wa Daraja la Mwiti (m 84) unatekelezwa kwa muda wa miezi 30.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tandahimba Ahmad Katani ameishukuru Serikali kwa mradi wa barabara hiyo kwani ni barabara ya kiuchumi kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Korosho.











 


Na Mwandishi Wetu, Tanga

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara Mkoani Tanga baada ya Mkandarasi kutoka China kushindwa kutimiza masharti ya mkataba. 

Mkandarasi huyo, kampuni ya China Railway 15 Bureua Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja - Mkange (km 95.2) wilayani Pangani anadaiwa kushindwa kufanya kazi aliyotakiwa kuifanya kwa wakati ingawa tayari amelipwa fedha yote na serikali. 

Baada ya kuvunja mkataba wa awali, Waziri Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kuondoa kilometa 25 za barabara hiyo ambazo hajazifanyiwa kazi na badala yake itangazwe zabuni mpya ili wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo wapewe kazi na waanze haraka. 

Kufuatia agizo hilo, sasa kilometa 25 za barabara hiyo na kilometa 70 za barabara inayoanzia Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) zitaunganishwa kwenye zabuni ili apatikane Mkandarasi wa kuijenga.

Ulega ametoa maelekezo hayo leo Mei 12, 2025 kwenye ziara yake Mkoani Tanga ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ambayo Serikali imekwishamlipa Mkandarasi kiasi cha shilingi Bilioni 47 ingawa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 48 tu.

“Mkandarasi huyu ametuangusha na hapa sisi hadai hata senti kwani tushamlipa zaidi ya bilioni 40, yupo nyuma ya muda, vifaa hajavileta vyote, wafanyakazi hawajawaleta wote, hivyo nimechukua maamuzi ya kumnyang’anya sehemu ya kazi ya mradi ili mradi huu ukamilike kwani ni wa muda mrefu na ni kilio cha wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kiujumla”, amesisitiza Ulega.

Ulega ameendelea kusisitiza kuwa maamuzi hayo ya kumyang’anya mkandarasi sehemu ya kazi ni kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi kwasababu Serikali ingeamua kuvunja mkataba wote ingechukua zaidi ya miezi 6 hadi mwaka mzima mpaka Mkandarasi mpya aanze kazi na hasara yake mradi kuendelea kuchelewa.

Vilevile, Ulega amemtaka Mkandarasi huyo kuilipa fidia Serikali kwa kuchelewesha mradi huo ambapo ameielekeza timu wa wataalam kuendelea kuchambua kimkataba juu ya hatua zitakazochukuliwa. 

Ulega amemwagiza Katibu Mkuu huyo kumweka mkandarasi huyo katika orodha ya Wakandarasi wasiofanya kazi vizuri katika miradi ya ujenzi kwa siku za usoni ili iweze kusadia wakati wa kupata Makandarasi wengine katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.

Kuhusu kilometa 70 ambazo Mkandarasi atatakiwa kuzimalizia, Ulega ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuisimamia kampuni hiyo ya China Railway 15 Bureua Group kufanya kazi usiku na mchana ili azikamilishe kuzijenga kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na ikiwa Wataalamu hao watashindwa kuwasimamia kikamilifu na wao watabadilishwa.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi kutoka TANROADS, Mhandisi Julius Msofe ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 47.82 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 100 na kuongeza kuwa muda wa mkataba wa miezi 36 sawa na asilimia 100 umeisha tangu tarehe 31 Machi 2025.










 Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha unatoa kipaumbele kwa vijana wazawa katika ujenzi wa miradi ya barabara inayoendelea nchini ili kupata ajira, kukuza ujuzi na uchumi kwa watanzania.


Akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndungu wilayani Same katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi China Communication Construction Company (CCCC), anayejenga barabara ya Ndungu-Mkomazi KM 36 kwa kiwango cha lami Waziri Ulega amesema ujenzi wa barabara hii itaondoa kero ya usafiri na usafirishaji ya siku nyingi na kuimarisha shughuli za kilimo, utalii na biashara.

"Rais Samia ametoa zaidi ya bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ili kuwakomboa wananchi kiuchumi hivyo ongezeni uzalishaji wa mpunga, tangawizi, ndizi na kukuza biashara kati ya Same, Korogwe na mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam", amesema Waziri Ulega.

Aidha amewataka TANROADS kusimamia na kuhakikisha barabara hii inajengwa usiku na mchana kwa ubora uliokusudiwa.

"Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amenituma Same nije niwatengezee barabara ili mlime tangawizi na mpunga kwa wingi kwa sababu anafahamu ninyi ni wachapakazi", amesisitiza Ulega.

Amesema inatarajiwa kuwa shughuli za kiuchumi za wananchi wa Same na Korogwe zitaimarika hivyo amemhimiza Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wahamasisheni vijana kuchangamkia fursa katika ujenzi huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema ujenzi wa barabara hiyo inayopita kwenye eneo lenye idadi kubwa ya watu wilayani humo itarahisisha maisha na kuibua fursa nyingi za uchumi wa watu wa Same.

Naye Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela amesema wananchi wa Same wanatoa machozi ya furaha, kwani shida kubwa inayowakabili ni barabara hivyo ujenzi wake ni ukombozi mkubwa kwa maisha yao.

" Leo mama Samia Suluhu Hassan anaandika historia ya kuikomboa Wilaya ya Same kwa kujenga barabara ya lami na ujenzi wake ukikamilika utaongeza uzalishaji wa mazao ya tangawizi, ndizi, matunda na mpunga", amesema Kilango.

" Mhe Ulega asilimia 72 ya tanggawizi inayozalishwa Tanzania inatoka Same hivyo barabara hii itarahisisha usafiri na usafishaji na kuwawezesha wananchi kuyafikia masoko kwa urahisi", amesisitiza Kilango.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema barabara ya Ndungu-Mkomazi Km 36 ni sehemu ya barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi yenye urefu wa Km 100.5 ambayo ni barabara ya kimkakati inayounganisha mkoa wa Tanga na Kilimanjaro ambapo km 96.5 ziko mkoa wa Kilimanjaro na Km 4 ziko mkoa wa Tanga hivyo kukamilika kwake kutachochea shughuli za kilimo, uvuvi, biashara na utalii katika hifadhi ya mkomazi na milima ya Pare.







 


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura iliyo chini yake. 

Waziri Ulega ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wake na Menejimenti na Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini  uliofanyika mjini Dodoma ambapo aliwaambia miradi ya dharura inapaswa kushughulikiwa kidharura. 

"Fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususan kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa”, amesema Ulega.

Ulega amewaambia mameneja hao kuwa wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.

Ulega alisema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na zile za El Niรฑo zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka. 

Mkutano wa Dodoma ulikuwa ni wa kwanza kwa Ulega kukutana na viongozi wa TANROADS tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais Samia Suluhu Hassan mwezi huu. 

Waziri huyo mpya alitumia nafasi hiyo kupongeza wafanyakazi wa wakala hiyo kwa  kufanya kazi kwa bidii na weledi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imekamilisha ujenzi wa barabara zaidi ya Kilometa 1,198 kwa kiwango cha lami.

Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, amewataka mameneja hao kufanya kazi kwa kujiamini na weledi mkubwa ili kuleta tija na ufanisi katika Sekta ya Ujenzi nchini ili kuondoa kero ya miundombinu mibovu kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Aidha, Ulega ametoa rai kwa Mameneja wa Mikoa yote nchini kuhakikisha maeneo yote yenye msongamamo wa magari hususani kwenye majiji na Manispaa yanafanyiwa usanifu yakinifu kwa ufasaha kulingana na mahitaji ya sasa na miaka mingi ijayo na kuratibiwa vizuri ili kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao kwa wakati.

Waziri Ulega amewahakikishia Mameneja hao kuwa Serikali awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Wakandarasi ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kasi ili kuendana na malengo ya Serikali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara kuu, za mikoa na madaraja yanajengwa ili kupitika wakati wote wa mwaka.

Balozi Aisha amewataka Mameneja wa TANROADS kuboresha usimamizi wa miradi, kulinda hifadhi za barabara pamoja na kupendezesha miji kwa taa za barabarani na utunzaji wa mazingira pembezoni mwa barabara.












Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) iimeeleza itaendelea kufanya kazi kwa bidii kila siku ili kuhakikisha miundombinu yake ya barabara na madaraja inakuwa bora na fursa kwa watumiaji wa ndani na nchi jirani za Jumuia ya Afrika Mashariki na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kauli hiyo imetolewa leo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta  katika mkutano wa 17 wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Sekta ya Uchukuzi unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba, 2024.

“TANROADS ni taasisi muhimu katika uwezeshaji wa usafiri na usafirishaji nchini ambapo tumeendelea kufanya kazi kwa bidii sana ili kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa bora zaidi, kwa kusimamia miradi mikubwa yote ambayo ni chachu ya maendeleo katika uchumi wa nchi yetu,” amesema Mha. Besta.

Mha. Besta amesema malengo ya TANROADS ni pamoja na kukuza ubora wa barabara katika majiji kwa kujenga madaraja ya juu na kufanya upanuzi wa barabara kuu zinazoingia katika majiji makuu, zikiwemo za Jiji la Arusha, ambapo sasa wanakamilisha usanifu wa barabara ya Arusha hadi Tengeru na USA River, na katika mkoa wa Kilimanjaro ujenzi wa barabara ya Kibosho na daraja la Kikavu na kwa Jiji la Mwanza barabara unganishi ya Usagara kwenda daraja la J.P Magufuli na upanuzi wa barabara ya Ubungo hadi Kimara kwa Jiji la Dar es Salaam.

Amesema pia TANROADS itaendelea kujenga madaraja ya juu katika Jiji la Dar es Salaam eneo la makutano ya Morocco na Mwenge, pia yatajengwa Jijini Arusha na sehemu nyingine nchini, na yote haya yanafanyika na kusaidia wananchi wanapata usafiri wa haraka.

Hatahivyo, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazitunza kwa kufuata viwango vilivyowekwa vya uzito wa magari na kutozidisha uzito kwenye magari ya mizigo, na kuacha tabia ya kutoa alama za barabarani kwa kuzifanyia matumizi mengine ambayo hayajakusudiwa, maana wanahatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hizo.

 


Kukamilika kwa uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songea kumefanya Mkoa wa Ruvuma kuwa kitovu muhimu cha biashara kwani idadi ya abiria imeongeza kutoka abiria 3,000 hadi kufikia 19,000 wanaoshuka Mkoani Ruvuma kwa kuwa hivi sasa ndege zinashuka mara tatu (3) kwa wiki. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo Septemba 23, 2024 katika Kilele cha Tamasha la Tatu la Utamaduni lililofanyika katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma.

“Nimeridhishwa sana na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea uliofanyika na kwamba Songea sasa inakwenda kuwa kitovu muhimu cha biashara kwasababu idadi ya wanaokuja Songea imeongezeka sana”, Amesema Dkt. Samia. 

Dkt. Samia ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuchangamkia fursa zinazotokana na uwepo wa Kiwanja hicho cha Ndege cha Songea.

Dkt. Samia ameeleza kuwa tangu mwaka 2021 Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo ya kijamii ikiwemo Shule, Hospitali, Maji pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa itakayokuza uchumi ikiwemo barabara, bandari, Kilimo na Madini.

 


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja katika eneo la Jangwani jijini Dar es salaam ambapo mkataba unatarajiwa kuwa umesainiwa mwezi Septemba, 2024.

Bashungwa ameeleza hayo leo Septemba 02, 2024 jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga aliyehoji Lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Daraja la Jangwani kuanzia Magomeni-Jangwani-Fire ili kuondoa adha wanayopata wananchi wakati wa mvua?

“Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imepanga kujenga Daraja katika eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita 15 ambapo hivi sasa taratibu za manunuzi zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wake”, ameeleza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja la Jangwani utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa ujenzi wa Daraja la Jangwani utaenda sambamba na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia mradi wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II).

Katika hatua nyingine, Bashungwa ameeleza kuwa tayari Wizara ya Ujenzi imeanza kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa Wakandarasi ambao walikuwa wakisubiria fedha hizo ili waweze kuendelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya barabara na madaraja inayoendelea na kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge fedha hizo zitaanza kutolewa mara moja ili kazi ziendelee.

1000267651

Watumishi wa Idara na Vitengo mbalimbali vya Makao Makuu ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), wamenolewa kwa kupata mafunzo yanayohusu utoaji na upokeaji wa rushwa kutoka kwa wadau mbalimbali.

Mwenzeshaji, Bi. Felista Banda, ambaye pia ni Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi wa TANROADS, amesema mada hii ni muhimu kufundishwa mara kwa mara kwa kuwa inawakumbusha watumishi katazo la upokeaji au utoaji rushwa, kwani kufanya hivyo kunadhoofisha utendaji kazi wa mtumishi husika na taasisi kwa ujumla.

Bi. Banda serikali kupitia taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Oktoba mwaka 2023 umezindua mkakati na mpango wa utekelezaji wa awamu ya nne utakaofanya kazi hadi mwaka 2030, ukiwa na lengo la kukuza uadilifu na kupambana na rushwa nchini.

1000267655

Amesema kwa upande wa TANROADS umeunda kamati ya uadilifu itakayoshughulikia masuala yote yanayohusiana na uadilifu katika taasisi ikiwemo ya watumishi watakaobainika kufanya vitendo vya upokeaji na hata utoaji rushwa kwa ajili ya kupata huduma fulani, kwa kutofuata taratibu kwa manufaa yao binafsi.

Bi. Banda amesema kamati hii ya uadilifu imeandaa mpangokazi wa kutekeleza kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kubainisha maeneo yenye viashiria vya rushwa na kuandaa afua za kushughulikia changamoto hizo ndani ya taasisi.

“Kamati ya uadilifu baada ya kumaliza kazi endapo itapata watumishi wenye kuvunja miiko na uadilifu kwa serikali wanawajibu wa kuwasilisha kwenye menejimenti ya taasisi kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi na kutolewa maamuzi,” amesema Bi. Banda  

Mbali na masuala ya rushwa pia watumishi wamefundishwa madili ya utendaji kupitia kanuni nane za maadili katika utendaji kazi wa utumishi wa umma, wanazopaswa kuzifuata zikiwemo za kutoa huduma bora, utii kwa serikali na kutuma huduma bila upendeleo.
 
  “Hizi kanuni zinatukumbusha watumishi wa umma kama vile serikali inavyotutaka kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa jamii, hivyo hatuna budi kuziishi bila kuzivunja au kuzikiuka ili serikali iweze kutoa huduma bora kupitia taasisi yetu ya TANROADS kwa jamii,” amesema Bi. Banda
1000267653
1000267649