Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuanza kutumika kwa daraja la Kigongo- Busisi kunatarajiwa kuimarisha na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji ndani na nje ya nchi na kuondoa changamoto ya upotevu mkubwa wa muda uliokuwepo awali kutokana na miundombinu iliyokuwepo.
"Hili daraja ni njia fupi ya kumfikisha mtu Bukoba mkoani Kagera leoleo kwa wakati muafaka, wakati zamani mtu akitaka kwenda Bukoba kabla ya maendeleo makubwa ya barabara katika nchi yetu hayajafika alikuwa lazima aende mpaka Kenya na Uganda kisha uingie Tanzania. Kwenda Bukoba ilikuwa lazima uende nchi mbili za jirani, tumeondoa unyonge huo." Ameeleza Waziri Ulega.
Leo Jumapili Juni 08, 2025 katika mjadala wa #MamaNiMjenzi, wenye lengo la kuangazia mafanikio ya miaka minne ya sekta ya Ujenzi nchini, Waziri Ulega ameeleza kuwa daraja hilo pia litaunganisha mikoa ya Mwanza, Geita, Kigoma, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Burundi, akisema Daraja hilo ni miongoni mwa viungo vitakavyokuza utengamano wa Afrika ya Mashariki.
Katika Mjadala huo ulioongozwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, Waziri Ulega amebainisha kuwa kutokana na daraja hilo kuwa na sifa za Daraja la Kitaifa, wamewaalika pia Mabalozi kutoka nchi jirani ili kuweza kushiriki katika uzinduzi wa daraja hilo baadae mwezi huu.
Post A Comment: