Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema katika Historia ya Tanzania, ni serikali ya awamu ya sita pekee inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyoweka fedha na mkazo mkubwa zaidi katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji kote nchini Tanzania.
Mhe. Ulega amebainisha hayo leo Jumapili Juni 08, 2025 Jijini Mwanza katikati ya Daraja la Kigongo- Busisi, miongoni mwa madaraja makubwa zaidi barani Afrika, likianzishwa ujenzi wake na hayati Dkt. John Pombe Magufuli kabla ya kuhitimishwa kwake na Rais Samia ambaye alipoingia madarakani alilikuta daraja hilo likiwa na asilimia 25 pekee katika utekelezaji wake.
"Rais Samia amekuwa muungwana sana hili daraja la Kigongo Busisi alilikuta asilimia 25 na yeye amelikamilisha, ilikuwa imelipwa kama Bilioni 130 tu hela ya awali, amelipa zaidi ya Bilioni 500 yeye mwenyewe na amelipa katika nyakati ngumu sana zile za Corona na ndiyo maana alipewa tuzo mwaka 2022 na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwasababu ya uimara wake kwenye nyakati ngumu." Amesema Waziri Ulega.
Waziri Ulega pia katika Mjadala wa pamoja na wanahabari wakati wa tathmini ya miaka minne ya Rais Samia ya #MamaNiMjenzi, amebainisha kuwa kwenye upande wa barabara za kiwango cha lami, miaka minne ya Rais Samia Jumla ya Kilomita 1,366 zimekamilika na zipo Kilomita nyongine 2,384 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wake.
Aidha katika historia ya Tanzania, Waziri Ulega amebainisha kuwa ni serikali ya Rais Samia ambayo inatekeleza mradi wa ujenzi wa vivuko vitano kwa wakati mmoja katika Ziwa Viktoria, akibainisha kuwa yote hayo yanafanyika kama sehemu ya kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini.
Post A Comment: