







Na Amiri Kilagalila,Njombe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 zitakazo fanyika mkoani Njombe tarehe mbili mwezi April.
Katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu Prof. Jamal Katundu ametoa taarifa hiyo mkoani Njombe mara baada ya kukagua uwanja wa Sabasaba uliopo mjini Njombe kutakapofanyika sherehe hizo.
“Ukiangalia uwanja zaidi ya 90% umekamilika kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwapongeza Njombe na kuwaomba wananchi mjitokeze kwa wingi tarehe mbili katika uzinduzi wa mbio za mwenge.tunategemea mgeni rasmi atakuwa makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Philip Mpango”alisema Katundu
Prof. Katundu amesema ameridhishwa na hali ya maandalizi inayoendelea ambapo amepongeza kamati za maandalizi za mkoa wa Njombe kwa kuandaa maonesho ya wajasiriamali ambayo yameanza ikiwa ni siku chache zimebaki kabla ya siku ya uzinduzi wenyewe.
“Kwa mara ya kwanza wanaNjombe wamejiongeza,kabla ya kufikia kilele watakuwa na shughuli mbali mbali za kibiashara tuwaombe pia watu wajitokeze kwenye hayo maonesho”aliongeza Katundu
Wakazi wa mkoa huu wameendelea na shughuli mbalimbali za maandalizi huku wakihamasishana kujitokeza kwa wingi. Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzinduliwa Mkoani Njombe kwa mwaka huu 2022 ukiwa na kauli Mbiu “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo Shiriki Kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akisisitiza jambo kwa Viongiozi wa Mkoa wa Njombe na Kamati ya Mkoa alipofanya ziara ya kukagua Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Sabasaba. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bi. Judica Omari. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Kasongwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (wa pili kutoka kushoto) akiwa ameongozana na Viongiozi wa Mkoa wa Njombe na Kamati ya Mkoa alipofanya ziara ya kukagua Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Sabasaba Februari 23, 2022. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mhandisi Marwa Rubirya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akikagua sehemu ya ukoka katika uwanja wa Sabasaba alipotembelea kwa lengo la kukagua Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amepongeza Kamati ya Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa hatua nzuri waliyofikia kuelekea katika uzinduzi wa tukio hilo muhimu linalotarajiwa kufanyika Aprili 2, 2022 Mkoani Njombe.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye kamati hiyo, Waziri Ndalichako alieleza kuridhishwa na hatua za awali za maandalizi na kuipongeza kamati ya Mkoa kwa kuendelea kusimamia na kuratibu vyema shughuli hiyo ya maandalizi.
“Kwa namna maandalizi haya yanavyoendelea vizuri inadhihirisha kuwa tulifanya maamuzi sahihi kuteua Mkoa wa Njombe kuwa ni sehemu ambayo Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa,”
“Hongereni kwa maandalizi ambayo mmefanya mpaka sasa na niwapongeze kwa kuonyesha utayari wa kuhakikisha shughuli hii ya kitaifa inafana, maana maandalizi mazuri yataleta heshima kwa Mkoa huu, hivyo mzingatie masuala yote ya msingi yatakayofanya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Njombe una kuwa wa kihistoria,” alisema Waziri Ndalichako
Aliongeza kuwa, kila mwaka Mwenge wa Uhuru hukimbizwa katika Mikoa, Wilaya na Halmashauri zote nchini ikiwemo Bara na Visiwani.
Waziri Ndalichako alifafanua kuwa Serikali imepanga kufanya Sensa ya Wat una Makazi mwezi Agosti 2022, hivyo kauli mbiu ya Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2022 ni; Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo; Shiriki Kuhesabiwa, Tuyafikie Maendeleo ya Taifa.
Sambamba na hayo Mheshimiwa Ndalichako aliwasihi wajumbe wa Kamati hiyo ya Mkoa kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao katika shughuli hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani humo.
Pia, Waziri Ndalichako alipokeza Mkoa kwa namna umekuwa ukishirikisha wadau ili waweze kujitokeza na kuchangia ufanikishaji wa shughuli hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mhandisi Marwa Rubirya alisema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema na maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru na aliahidi kusimamia shughuli zote za maandalizi kwa ufanisi na kukamilisha ndani ya muda uliopangwa.
“Nikuhakikishie uteuzi huu tutautendea haki na tutawezesha wananchi wa Mkoa wa Njombe wanashiriki katika tukio hilo muhimu na kutumia fursa hiyo ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kujitangaza kama Mkoa,” alisisitiza Mhe. Rubirya
Katika ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alitembelea Uwanja wa Sabasaba ambapo uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kufanyika, pia aliwatembelea vijana wa Halaiki katika Shule ya Sekondari Mpechi Mkoani Njombe.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
OWM - KVAW