Watanzania wameaswa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 litakayofanyika nchi nzima Agosti 14, 2022.

Akizungumza jana mkoani Njombe wakati akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema kuwa lengo la Serikali la kufanya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni kupata takwimu zitakazoisaidia katika uandaaji wa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

“Ninawasihi sana Watanzania mjitokeze na kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi na taarifa zitakazokusanywa zitakuwa siri na zitatumika kwa ajili ya matumizi ya Sensa peke yake” Alisisitiza Makamu wa Rais

Aidha, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango amewataka waratibu na viongozi mbalimbali kuwaandaa wananchi nchi nzima ili waweze kushiriki zoezi la Sensa.

“Naamini wananchi wakiwa na uelewa wa kutosha watatoa ushirikiano unaohitajika, hivyo nawaomba viongozi wote wa Vyama vya Siasa, dini na Serikali muelimishe wananchi umuhimu wa kuhesabiwa” Alisisitiza Makamu wa Rais.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa baada ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 vijana sita waliondaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, wataukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mikoa 31 na halmashauri 195 nchini kwa siku 195.

“Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao ambapo ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu umezingatia, hoja, na vipaumbele vya Serikali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kauli mbiu ya Mwenge mwaka huu ni Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa”. Alisema Profesa Ndalichako.
Share To:

Post A Comment: