Na Amiri Kilagalila,Njombe


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022 zitakazo fanyika mkoani Njombe tarehe mbili mwezi April.

Katibu mkuu ofisi ya waziri mkuu Prof. Jamal Katundu ametoa taarifa hiyo mkoani Njombe mara baada ya kukagua uwanja wa Sabasaba uliopo mjini Njombe kutakapofanyika sherehe hizo.

“Ukiangalia uwanja zaidi ya 90% umekamilika kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwapongeza Njombe na kuwaomba wananchi mjitokeze kwa wingi tarehe mbili katika uzinduzi wa mbio za mwenge.tunategemea mgeni rasmi atakuwa makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Philip Mpango”alisema Katundu

Prof. Katundu amesema ameridhishwa na hali ya maandalizi inayoendelea ambapo amepongeza kamati za maandalizi za mkoa wa Njombe kwa kuandaa maonesho ya wajasiriamali ambayo yameanza ikiwa ni siku chache zimebaki kabla ya siku ya uzinduzi wenyewe.

“Kwa mara ya kwanza wanaNjombe wamejiongeza,kabla ya kufikia kilele watakuwa na shughuli mbali mbali za kibiashara tuwaombe pia watu wajitokeze kwenye hayo maonesho”aliongeza Katundu

Wakazi wa mkoa huu wameendelea na shughuli mbalimbali za maandalizi huku wakihamasishana kujitokeza kwa wingi. Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzinduliwa Mkoani Njombe kwa mwaka huu 2022 ukiwa na kauli Mbiu “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo Shiriki Kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa.”

Share To:

Post A Comment: