Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20, 2025, Jijini Dodoma
Na Alex Sonna, Dodoma
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha kampasi mpya zinazoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali zinajielekeza katika kutoa mafunzo ya ujuzi (Amali), ili kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea na kushindana katika soko la ajira.
Agizo hilo limetolewa leo Januari 20,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati wa kikao kazi cha kimkakati kati ya Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini yake, kilicholenga kujadili utekelezaji wa majukumu na malengo ya sekta hiyo.
Prof. Mkenda amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 inaelekeza kwa nguvu zote kuandaliwa kwa wahitimu wenye ujuzi, hivyo ni muhimu kampasi mpya zikabeba dhana ya mafunzo ya amali kama ufundi na ufundi stadi.
“Haya ni maagizo ya Sera. Tunapopanua miundombinu ya elimu ya juu, lazima tuhakikishe tunapanua pia ujuzi kwa vitendo. Kampasi hizi mpya zisigeuke kuwa za kufundisha nadharia pekee, zizingatie mafunzo ya amali kwa lengo la kuongeza tija kwa Taifa,” amesema Prof. Mkenda.
Aidha Prof.Mkenda amesema kuwa serikali imeanza kuchukua hatua mahsusi za kutatua changamoto ya upatikanaji wa ufadhili wa masomo nje ya nchi baada ya kubaini kuwa wanafunzi wengi wa Kitanzania wanakosa fursa hizo kutokana na kushindwa kuziomba ipasavyo.
Prof. Mkenda amesema Serikali imefanikiwa kupata nafasi 127 za ufadhili wa masomo nchini Saudi Arabia, lakini bado idadi ya wanafunzi wanaoomba na kunufaika na fursa hizo ni ndogo, hali iliyosababisha Wizara kuanza kushughulikia vikwazo vinavyowafanya wanafunzi wengi kushindwa kuomba masomo nje ya nchi.
Amesema Wizara imeanza mchakato wa haraka wa kufanya tathmini ili kubaini sababu zinazofanya Watanzania kutozitumia kikamilifu fursa za masomo nje ya nchi pindi zinapojitokeza, akisisitiza kuwa hali hiyo haikubaliki ikizingatiwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata elimu katika vyuo vya nje ya nchi.
“Ni muhimu kubaini kwa nini fursa zinapopatikana hazichangamkiwi na Watanzania, ili Serikali iweze kuchukua hatua sahihi na kuongeza ushiriki wa wanafunzi wetu katika masomo ya kimataifa,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kuwa kikao hicho ni fursa muhimu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa sera na mipango ya Wizara.
Aidha amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa Wizara, taasisi zake na wataalamu wa sekta ya elimu ili kuhakikisha mageuzi yanayopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Naye ,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kikao hicho cha kimkakati kimewaleta pamoja viongozi wa wizara na taasisi ili kupitia utekelezaji wa malengo ya mwaka 2025/26 na kupanga mikakati itakayowezesha kufikiwa kwa Dira 2050 katika sekta za Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Amesema mikakati hiyo inajumuisha utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, uimarishaji wa mafunzo ya amali katika ngazi ya sekondari, kuimarisha fursa za elimu ya juu pamoja na masuala ya ufadhili.
“Tutajadili pia programu nyingine muhimu zenye lengo la kuboresha sekta ya elimu, kuimarisha ubora, usawa na upatikanaji wa huduma kwa Watanzania wote,” amesema Prof. Nombo.
Kikao hicho kinatarajiwa kutoa mwongozo mpya wa utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali katika sekta ya elimu kuelekea kufikiwa kwa malengo ya muda mfupi na mrefu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20, 2025, Jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20, 2025, Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20,2026 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Hussein Omary,akifuatilia mada mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20,2026 jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi,akifuatilia mada mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika leo Januari 20,2026 jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma.

















.jpg)
.jpg)








.jpg)