Serikali mkoani Kilimanjaro imeanza utekelezaji wa mkakati maalum wa kuwawezesha maafisa ugani kupitia mafunzo ya kitaalamu, ikiwa ni jitihada za kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.


Hatua hiyo inalenga pia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuinua kipato cha wakulima katika mkoa huo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), yaliyofanyika Machi 17, 2026 katika ukumbi wa Manispaa ya Moshi, Katibu Tawala Msaidizi wa Kilimo na Ufugaji, Dkt. Emmanuel Lema alisema maafisa ugani wanapaswa kutumia mbinu za kisasa na ubunifu ili kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maafisa hao ili waweze kushauri matumizi sahihi ya mbegu bora, teknolojia za kisasa za kilimo pamoja na mbinu za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.


Aidha, Dkt. Lema alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, kusambaza pembejeo na kuwapatia maafisa ugani vitendea kazi vinavyohitajika. Pia aliwataka maafisa hao kushiriki kikamilifu katika kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Kwa mujibu wa takwimu za mkoa, Kilimanjaro imezalisha tani 1,259,115 za mazao ya chakula katika mwaka wa kilimo 2024/2025, kiwango kinachozidi mahitaji ya tani 773,115.


Naye Afisa Kilimo kutoka COPRA, Bi. Paskalia Sitembela alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa mafunzo yatakayochochea uzalishaji wa mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.


Maafisa ugani walioshiriki mafunzo hayo wameahidi kuyatumia ipasavyo ili kuwafikia wakulima katika maeneo yao na kuwapatia elimu sahihi ya kilimo, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wenye tija katika mkoa na taifa kwa ujumla.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: