Na. Josephine Majura na Peter Haule, WF, Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Devotha Minja, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kutekeleza Mradi wa Jengo jipya la Ofisi ya Wizara lililopo Mji wa Serikali Mtumba, kwa ufanisi, kwa kuwa mradi huo hauna maswali mengi ikilinganishwa na miradi mingine waliyoitembelea.
“Kazi ni nzuri, mmefanya kazi kubwa na taarifa zinazohitajika ziwasilishwe ili tuweza kuishauri vema Serikali”, alisema Mhe. Minja.
Aidha Mhe. Minja kwa niaba ya Kamati ameahidi kutoa ushirikiano katika maeneo mbalimbali yanayoihusu Wizara ya Fedha kwa Maendeleo ya Wananchi.
Akizungumza na Ujumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya PAC, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula (Mb) alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la hilo lenye mvuto wa kipekee katika eneo hilo likiwa na urefu wa ghorofa tisa.
Mhe. Luswetula alisema kuwa jengo hilo lililofikia hatua ya asilimia 98 katika utekelezaji wake, anaimani watumishi wa Wizara ya Fedha wataongeza morali ya kazi kutokana na mazingira bora ya kazi katika jengo hilo lenye hadhi kubwa.
“Kwa mazingira haya majukumu ya Wizara ya Fedha yataenda vizuri ikiwa ni pamoja na utatuzi wa changamoto za wananchi wote kwa ujumla”, alisema Mhe. Luswetula.
Mhe. Luswetula alimhakikishia Mwenyekiti wa Kamati ya PAC kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa ikiwemo kuwasilisha taarifa za jengo hilo kwa ujumla wake.
Kamati ya Kudumu ya PAC imetembelea mradi wa Jengo hilo na kukagua Ofisi mbalimbali zikiwemo za Viongozi na Watumishi wa Wizara, Mifumo ya Fedha, usalama wa jengo, masuala ya Afya, kumbi za Mikutano na maeneo mengine.
.jpg)
Post A Comment: