NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), imefanikiwa kukamata jumla ya paketi 753 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni zilizofanyika Tanzania na Kenya, huku watuhumiwa saba wakikamatwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 9, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema operesheni hizo ni sehemu ya juhudi za kuvunja mitandao ya kimataifa inayojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Amesema katika operesheni ya kwanza iliyofanyika Novemba 6, 2026, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, mamlaka hiyo ilikamata paketi 299 za dawa za kulevya, zikiwemo 24 za heroin na 275 za methamphetamine.
Amesema dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo pia yalikamatwa kutokana na kuhusishwa na uhalifu huo.
Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa ambao ni Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda, pamoja na Issa Said Nassoro (34), Ibrahim Said Chembela (30) na Mohamed Ally Shemtuu (45), wakazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Lyimo, maelezo ya awali ya watuhumiwa yalionesha kuwa dawa hizo zilichukuliwa Mombasa nchini Kenya na kusafirishwa kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga.
Amesema kutokana na taarifa hizo, DCEA ilishirikiana na mamlaka za Kenya kufanya uchunguzi zaidi, hatua iliyowezesha kubaini chanzo cha dawa hizo na kuwafuatilia wahusika wengine wa mtandao huo.
Uchunguzi huo ulisababisha operesheni nyingine kufanyika Novemba 7, 2026, katika eneo la Kwale, Mombasa nchini Kenya, ambapo DCEA kwa kushirikiana na NANB ilikamata paketi nyingine 454 za methamphetamine na kuwakamata watuhumiwa watatu.
Watuhumiwa hao ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu Mbwiga, Seif Said Hamad (54), maarufu Babu Seif, na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wanadaiwa kuwa vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya unaofanya shughuli zake katika nchi mbalimbali zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.
Saleh Khamis Baseleman, maarufu Mbwiga, anadaiwa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi katika fukwe za Mombasa nchini Kenya kabla ya kuzisambaza katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.
Vilevile, mtuhumiwa huyo anahusishwa na ukamataji wa tani 3.5 za dawa za kulevya uliofanywa na DCEA Desemba 2023 katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Kwa upande mwingine, Lyimo amesema taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kubaini viashiria vya biashara na matumizi ya dawa hizo.

Post A Comment: