Mkuu wa wilaya ya Arumeru Bi. Neema Lugangira amesema uhusiano kati ya Tanzania na Italia unazidi kuimarika kupitia ushirikiano katika sekta za maendeleo, uhifadhi wa mazingira na diplomasia ya kibunge. 

Lugangira ameyasema hayo wakati akiipongeza Taasisi ya Oikos East Afrika  kwa kujitolea kuboresha ustawi wa jamii kupitia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kijamii kwenye hafla ya kumtunuku Dkt. Giorgio Colombo tuzo ya Nishani ya Nyota ya Italia katika daraja la Knight, aliyotunukiwa na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Coppola.

"Serikali inatambua mchango wa taasisi hii na itaendelea kuunga mkono mipango yenu, ila niwaombe muendelee kupanua huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wananchi wangu wa Arumeru ili muweze kuendeleza mafanikio yaliyopatikana." Alisema Lugangira

Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Coppola, amesema uwepo na mchango wa taasisi pamoja na raia wa Italia wanaofanya shughuli mbalimbali nchini Tanzania ni sehemu muhimu ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Italia unahusisha diplomasia ya kibunge, ambapo viongozi wa mabunge nchini Italia wameeleza umuhimu wa kuendeleza uhusiano kati ya wabunge wa mataifa haya kupitia Umoja wa Mabunge Duniani, unaojulikana kwa kifupi kama IPU.

Katika ngazi ya serikali za mitaa, ushirikiano huo umetajwa kuwa na mchango katika maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira, huku taasisi ya Oikos East Afrika ikihimizwa kuendelea kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa katika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Hata hivyo,  Dkt. Giorgio Colombo aliyetunikiwa tuzo ya Nishani ya Nyota ya Italia katika daraja la Knight,  amesema Oikos East Afrika  itaendelea kushirikiana na serikali, jamii na wadau wengine katika kuhimiza maendeleo yanayozingatia uhifadhi wa mazingira.

Amesisitiza kuwa juhudi za kuboresha maisha ya wananchi haziwezi kutenganishwa na utunzaji wa mazingira, akieleza umuhimu wa kuhakikisha jamii zinaishi katika mazingira salama na endelevu.

Tuzo hiyo iliyotolewa kwa niaba ya Rais wa Italia, Sergio Mattarella, inatambua mchango wa Dkt. Colombo katika ushirikiano wa kimataifa na maendeleo, hususan kupitia kazi zake katika taasisi ya Oikos East Afrika 

Kupitia taasisi hiyo, Dkt. Colombo ameshiriki katika juhudi za kuboresha upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira, huku uhifadhi wa mazingira ukiwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi katika jamii mbalimbali.














Share To:

Post A Comment: