Na OWM – TAMISEMI, Dodoma


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuhusu kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi inayosimamiwa na Ofisi hiyo.

Katika kikao hicho, pande hizo zimejadili maeneo ya ushirikiano, hususan matumizi ya utaalamu, teknolojia na uzoefu wa kitaasisi katika kuhakikisha miradi ya miundombinu inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa, kwa wakati na kuleta thamani halisi kwa wananchi.

Mhandisi Mativila amesisitiza umuhimu wa taasisi za Serikali kushirikiana na vyuo vikuu katika kupata suluhisho za kitaalamu zitakazosaidia kuongeza ufanisi na ubora wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Innocent Macho, alisema Chuo hicho kina uwezo na uzoefu mkubwa wa kutoa huduma za kitaalamu kupitia kampuni yake ya ushauri, The Bureau for Industrial Cooperation (BICO), ambayo imeshiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.

Pande hizo zimekubaliana kuendelea na majadiliano ili kuweka mazingira madhubuti ya ushirikiano yatakayochangia utekelezaji bora na endelevu wa miradi ya miundombinu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: