Na Mwandishi wetu -IRINGA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,  Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe.  Nderiananga amewapongeza watu wenye ulemavu kwa kushiriki shughuli za kiuchumi na kuongeza pato lao na Taifa kwa ujumla.


Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na watu wenye ulemavu  katika Kituo cha wenye ulemavu cha Neema Craft kilichopo Manispaa ya Iringa Mh. Ummy alisema kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha watu wenye ulemavukupata elimu, mafunzo ya ufundi na mitaji ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Pia aliongeza kuwa watu wenye ulemavu wanapopata elimu ya fani mbalimbali huwajengea hali ya kujiamini, kuwa tayari kuonyesha uwezo wao na kuwa wabunifu hatimaye kupunguza wimbi la utegemezi.

" Nikipongeze Kituo hiki cha Neema Craft kwa hatua kubwa waliopiga katika kuwawezesha wenye ulemavu kwenye ujuzi mbalimbali kama tulivyoona kuna ufundi seremala, ufumaji, ushonaji, upishi na fani nyingine nyingi ambapo zote hizi zinafanywa na watu wenye ulemavu kwetu kama Serikali ni furaha kubwa," Alipongeza Mhe. Ummy


Hata  hivyo amewataka watu wenye ulemavu kutumia fursa za mikopo, mafunzo na uwezeshaji zinazotolewa na Serikali ili kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi zitakazowasaidia kujitegemea.

"Wananchi wanaponufaika na mikopo hii ni heshima kubwa kwa Mbunge pia Mkuu wa Mkoa kaka yangu Kheri James nawapongeza sana kwa namna mnavyopambana kwa ajili ya watu wenye ulemavu," alisema.

Vile vile Mhe. Ummy alifafanua kwamba baadhi ya watu wenye ulemavu wameonyesha uwezo mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, zikiwemo samani, mikoba, mikeka na mazulia, huku bidhaa hizo zikiuzwa katika hoteli na masoko mbalimbali.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya shughuli zenye tija endapo watapata uwezeshaji unaostahili.

"Nimetembelea hapa Neema Craft nimejionea namna watu wenye ulemavu wanavyofanya shughuli zao za ujasirimali wanabuni na kutengeneza bidhaa nzuri ambazo hata watu wazima hawawezi na bidhaa hizo mara nyingi tunaziona katika mahoteli makubwa ambayo huwezi kuzania kwamba watu wenye ulemavu ndio wametengeneza,"Alieleza.

Aidha aliwataka wazazi na walezi kutowaficha ndani watoto wenye ulemavu badala yake kuwapeleka shule au vyuo vya ufundi na vituo vinavyotoa mafunzo ya ujuzi hatua itakayosaidia kujikwamua kiuchumi hatimaye kutoka katika hali ya kuwa omba omba mitaani.

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa Kituo cha Neema Crafts mkoani Iringa Bwa. Joseph Adams alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2003 ikiwa ni  mradi wa kijamii unaolenga kutoa mafunzo na ajira kwa watu wenye ulemavu kama vile wasiyosikia ( viziwi)  na wenye ulemavu wa viungo ili kuwapa heshima na kuwaepusha na kuomba barabarani. 


"Kituo hiki kinajumuisha kazi nyingi sana na zote wanafanya wao wenyewe na kuzalisha bidhaa ambazo tunaziuza kama vile Karakana za kazi za mikono, Mgahawa  unaoendeshwa na viziwi na  Nyumba ya wageni (Guesthouse),"Alisema  Mkurugenzi huyo.

Aidha aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuonyesha upendo kwa wenye ulemavu bila ubaguzi huku akiiomba kuboresha sekta ya wakalimani kuwasaidia wenye ulemavu kupata huduma muhimu kama hospitali, taasisi za fedha, nyumba za ibada na nyinginezo.


MWISHO

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: