Serikali imewaagiza wazalishaji wote nchini kutumia alama ya 'Made in Tanzania' ili kuongeza imani kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Agizo hilo limetolewa  na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Immanuel Nchimbi, kwenye kilele cha Usiku wa Jubilei ya Dhahabu (Miaka 50) ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), uliofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Sherehe hizo zilienda sambamba na utoaji wa tuzo kwa washirika muhimu wa mamlaka hiyo. Udhibiti wa Viwango na Huduma za Kifedha.

Aidha, Makamu wa Rais amezitaka taasisi zinazosimamia viwango na huduma za kifedha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakidhi viwango vya kimataifa. Alisema matumizi ya alama ya 'Made in Tanzania' yataongeza utambulisho wa bidhaa zenye ubora na kuimarisha heshima ya taifa katika biashara za kimataifa.

 "Nazipongeza taasisi za fedha kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo na vya kati, akisema hatua hiyo imeendelea kupunguza changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na kuchochea ukuaji wa uzalishaji nchini."amesema Balozi Nchimbi

Amesema Serikali itaendelea kuweka sera rafiki, kuboresha miundombinu na kuimarisha sekta binafsi ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani. Ameongeza kuwa maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya TANTRADE ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kuongezeka kwa viwanda, uzalishaji, ajira na upanuzi wa masoko ya bidhaa za Tanzania duniani.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesisitiza kuwa manufaa makubwa ya rasilimali zilizopo nchini yatapatikana Tanzania itakapowekeza katika kuchakata na kuzalisha bidhaa za mwisho zenye ubora wa juu badala ya kuuza malighafi ghafi nje ya nchi.

Waziri Kapinga amebainisha kuwa hatua hiyo itafungua masoko mapya, itaongeza thamani ya mauzo ya nje, na kuinua uchumi wa wananchi kwa ujumla.

Mhe. Kapinga ameeleza kuwa, ili kujenga uchumi imara wa viwanda na wenye ushindani, kuna haja ya kubadili mtazamo wa kibiashara kwa kuhakikisha mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini yanageuzwa kuwa bidhaa zilizofungashwa vizuri na kukidhi viwango vya kimataifa.

Amesisitiza kuwa uwekezaji mkubwa katika teknolojia za kisasa una mchango mkubwa katika kuongeza kiwango cha uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa zinazotengenezwa nchini, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuzipa bidhaa za Tanzania uwezo mkubwa wa kushindana katika soko la kimataifa.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: