Wafugaji nchini wanatarajiwa kunufaika na biashara ya kisasa ya mifugo baada ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuanza kuingiza mifugo katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, utakaounganisha taarifa za mifugo kidijitali na kuwawezesha wanunuzi kushindana kwa uwazi kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema baada ya mafanikio ya kusimamia bidhaa 18 za mazao ya kilimo kupitia mfumo huo, sasa bodi imepanua huduma zake kwa kujumuisha mifugo.

Amesema hatua hiyo inatokana na mahitaji ya wafugaji waliokuwa wakihoji kwa nini mfumo huo unawanufaisha wakulima pekee huku sekta ya mifugo ikibaki nje.

"Tumekuja na bidhaa mpya ambazo zimeongezwa kwenye mfumo, na kubwa zaidi tumewafikia wafugaji. Tulikuwa tunasimamia bidhaa 18 za mazao ya kilimo, lakini sasa tumeingia rasmi kwenye bidhaa za mifugo," amesema.

Bw. Bangu amesema WRRB inalenga kuunganisha biashara ya mifugo na TMX, ambapo taarifa za kila mnyama zitawekwa kidijitali ili wanunuzi waweze kuzifikia kwa urahisi, kushindana kwa uwazi na kufanya maamuzi ya ununuzi kwa kutumia taarifa sahihi badala ya makadirio.

Ameeleza kuwa mfumo huo utatumia taarifa zinazopatikana kupitia hereni za utambuzi wa mifugo zilizozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambazo zina namba maalumu zinazobeba taarifa za kila mnyama.

"Tunafahamu Mheshimiwa Rais Samia miaka miwili iliyopita alizindua uwekaji wa hereni kwenye mifugo. Sisi kama WRRB tunapiga hatua zaidi kwa kutumia taarifa zilizopo kwenye hereni hizo kuingiza mifugo kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Hereni hiyo ndiyo itakuwa msingi wa stakabadhi kwa kuwa ina namba na taarifa zote za mnyama," amesema.

Amefafanua kuwa mfumo huo utawanufaisha wafugaji wanaojishughulisha na unenepeshaji wa mifugo kwa kuwa mifugo yao itahifadhiwa katika maeneo maalumu yatakayokuwa yanatambulika kama ghala, huku wafugaji wakipewa stakabadhi zitakazowawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.

Kwa mujibu wa Bangu, WRRB tayari imefikia makubaliano na Benki ya NBC ambayo imekubali kutoa mikopo kwa wafugaji watakaoweka mifugo yao kwenye ghala.

"Wengi wanauliza ghala litakuwaje. Kwa upande wa mifugo, zizi ndilo litakuwa ghala. Mifugo itatunzwa katika maeneo maalumu yenye chakula na huduma za matibabu, huku mfugaji akiwa na stakabadhi inayomwezesha kupata fedha bila kulazimika kuuza mifugo yake mapema," amesema.

Bangu amesema hatua nyingine muhimu ni kuondoa utaratibu wa kupanga bei kwa kutazama mwonekano wa mnyama pekee, badala yake mifugo itapimwa kwa uzito ili bei iweze kuamuliwa kwa kuzingatia kilo halisi za mnyama.

"Leo hii kwenye minada mingi ng'ombe anapimwa kwa macho, anaonekana mnene au mwembamba ndipo bei inawekwa. Sisi tunataka mifugo ipimwe kwa uzito ili bei iwe ya haki kwa mfugaji na mnunuzi. Hii itakuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji na pia itarahisisha upatikanaji wa taarifa zinazohitajika katika masoko ya ndani na kimataifa," amesema.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: