Serikali imeahidi kuendelea kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani ili kuongeza uwezo wa uzalishaji na kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga(Mb), Julai 09, 2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ziara yake katika Kiwanda cha Kamal Refinery kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani kinachojihusisha na uchakataji wa mafuta machafu ya mitambo na magari (Waste/Used Lube Oil) ili kuyasafisha na kuzalisha mafuta mapya ya vilainishi (lubricants) na mafuta mazito ya viwandani (heavy fuel oil).
Aidha, amesema Sekta ya Viwanda na Biashara imeweka kipaumbele cha juu katika kuongeza minyororo ya thamani ya uzalishaji hapa nchini mkakati unaolenga kupunguza utegemezi na uingizaji wa bidhaa kutoka nje ambazo zina uwezo na sifa ya kuzalishwa kikamilifu na viwanda vya ndani.
Amesema uwekezaji huo umebainika kuwa na manufaa makubwa kimazingira, kwani unachangia kuweka mazingira katika hali ya usafi na usalama katika wakati ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa kinara na “Champion” wa utunzaji wa mazingira.
Aidha, amesema ili kufanikisha azma hiyo, Sekta ya Viwanda na Biashara itashirikiana kwa karibu na Wizara yenye dhamana ya Mazingira, ambayo tayari ina uhusiano wa kikazi na kiwanda hicho ili kuhakikisha kiwanda hicho kinaongeza uzalishaji na kukuza biashara huku kikizingatia kikamilifu utunzaji endelevu wa ikolojia.
Vilevile, Amewasihi wadau mbalimbali kuunga mkono kiwanda hicho, kinachosaidia kulinda mazingira ya taifa kwa vizazi vijavyo huku akiwataka Watanzania kuendelea kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bw. Sameer Santosh ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na kuwaunga mkono wazalishaji wa ndani.
Amesema kiwanda hocho kitaendelea kuongeza zaidi uwezo wa uzalishaji ili kupunguza uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.


Post A Comment: