Na. Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC), Dkt. Aggrey Mlimuka, ametembelea banda la FCC katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Maonesho hayo yamewakutanisha washiriki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo kampuni binafsi, taasisi na mashirika ya Serikali, yakitoa fursa ya kutangaza bidhaa, huduma na uwekezaji.

Akiwa katika banda la FCC, Dkt. Mlimuka ameipongeza Tume hiyo kwa kazi kubwa inayofanya katika kulinda ushindani wa haki sokoni na kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa bandia, hatua inayochangia kulinda maslahi ya walaji na kukuza mazingira bora ya biashara nchini.

Pia amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, Menejimenti pamoja na watumishi wote wa Tume hiyo kwa kujituma, weledi na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha taasisi hiyo inatimiza malengo yake kwa mafanikio.

FCC ina jukumu la kulinda na kuhimiza ushindani wa haki katika biashara, kulinda maslahi ya walaji, kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa sheria za ushindani, pamoja na kudhibiti uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa bandia nchini.

Mbali na kutembelea banda la FCC, Dkt. Mlimuka pia alitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kujionea shughuli na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yenye kaulimbiu "Sabasaba Fahari ya Tanzania," yalianza rasmi Juni 28, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Maonesho vya Julius Nyerere (Sabasaba Grounds), Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC) akipata maelezo kutoka kwa Bi. Roberta Feruzi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano - FCC wakati alipotembelea banda hilo katika maonesho ya 50 ya biashara ya Kimataifa  yanayoendelea viwanja wa Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa FCC wakati alipotembelea banda hilo katika maonesho ya 50 ya biashara ya Kimataifa  yanayoendelea viwanja wa Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: