Wizara ya Nishati imesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kufanikisha lengo la Taifa la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Wito huo umetolewa na Mjiolojia Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bw. Ngereja Mgejwa, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, wakati akifungua Maonesho na Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia 2026 (Clean Cooking Expo 2026), Juni 23, 2026 katika Ukumbi wa EACLC jijini Dar es salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo, Bw. Mgejwa amesema nishati safi ya kupikia ni ajenda muhimu ya kitaifa inayohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuleta mabadiliko ya kudumu katika sekta ya nishati. Amesema matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kulinda afya za wananchi, hususan wanawake na watoto, kuhifadhi mazingira, kuinua elimu kwa watoto wa kike na kuongeza tija ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa kazi iliyopo mbele ni kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia iliyo nafuu, salama na endelevu ikiwemo gesi oevu (LPG), majiko banifu, gesi asilia, umeme, bayogesi na bayoethanoli.

 Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati safi pamoja na kutoa elimu kwa umma ili kubadili matumizi ya nishati za jadi kwenda kwenye nishati safi.

Bw. Mgejwa amepongeza Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwa kuandaa kongamano hilo, akisema majadiliano yatakayofanyika yataibua suluhisho na mapendekezo yatakayochochea ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

 Ameongeza kuwa kongamano hilo litahitimishwa kwa Mbio za Nishati Safi ya Kupikia zitakazotumika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi kwa afya na uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania(TABWA) Bi. Noreen Mawalla amesema maonesho hayo yameandaliwa chini ya kaulimbiu ya "Linda Afya, Hifadhi Mazingira, Okoa Muda kwa Uchumi Endelevu" kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Amebainisha kuwa Clean Cooking Expo 2026 itafanyika kwa siku tatu na itajumuisha mafunzo, mijadala na maonesho ya teknolojia mbalimbali za nishati safi zitakazowakutanisha wadau kutoka sekta ya umma na binafsi. 

Amewakaribisha wananchi kutembelea mabanda ya maonesho ili kupata elimu na taarifa sahihi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku akieleza kuwa Mbio za Nishati Safi ya Kupikia zitafanyika Jumamosi na zinatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi.







Share To:

Post A Comment: