Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhe. Paschale Katambi Patrobas (Mb), aliyewakilishwa na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Afande Jeremiah Katungu Amewatunuku wafungwa 173 kati yao wanawake 6 na wanaume 167 vyeti vya mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara katika hafla ya mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara kwa ushirikiano wa Chuo Cha Uhasibu Arusha yaliyofanyika leo tarehe 22/June/2026 katika viwanja vya magereza kisongo mkoani Arusha.

Wakati wa utoaji wa vyeti hivyo Mhe. Katungu amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya marekebisho ya wafungwa kwa kuwekeza katika elimu na ujuzi unaowawezesha kuwa wananchi wenye tija wanaporejea katika jamii na kuongeza kuwa  mafunzo hayo yamekuwa nyenzo muhimu ya kuibua vipaji, kuongeza uwezo wa kujiajiri na kupunguza uwezekano wa kurudia vitendo vya uhalifu, huku akipongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Magereza na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika kufanikisha programu hiyo yenye manufaa makubwa kwa taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, amesema uwekezaji katika elimu ya ujasiriamali na stadi za biashara kwa wafungwa ni hatua muhimu ya kuwawezesha kujijengea maisha mapya yenye heshima na mchango chanya kwa jamii. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema chuo hicho kinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii kwa kutoa elimu na mafunzo yanayolenga kuleta mabadiliko chanya kwa makundi mbalimbali ya jamii,na kuongeza kuwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara yaliyotolewa kwa wafungwa yamewajengea uwezo wa kubuni, kuanzisha na kusimamia shughuli mbalimbali za kiuchumi, hatua ambayo itawawezesha kujitegemea na kuwa sehemu ya nguvu kazi ya taifa baada ya kumaliza vifungo vyao. Profesa Sedoyeka ameongeza kuwa IAA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa elimu inayojenga jamii jumuishi na yenye ustawi endelevu.

Utekelezaji wa mafunzo hayo kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Magereza na Chuo cha Uhasibu Arusha unakwenda sambamba na azma ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani.










Share To:

Post A Comment: