📌Washiriki Nishati Safi expo wafurahishwa na miradi ya REA
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeshiriki Maonesho na Kongamano la Nishati Safi expo 2026 yanayofanyika katika ukumbi wa Ubungo EACLC jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba.
Akizungumza katika kongamano hilo leo Juni 24, 2026, Msimamizi wa miradi ya REA, Mha. Francis Manyama amesema kuwa, upatikanaji wa umeme vijijini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuongeza matumizi ya nishati safi.
Ameongeza kuwa, miradi ya usambazaji wa umeme vijijini imewezesha wananchi kuachana na matumizi ya majenereta na vyanzo vingine vya nishati vinavyotumia mafuta, hali inayosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.
Halikadhalika, REA inaendelea na mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua katika visiwa mbalimbali nchini, ambapo mifumo 20,000 inatarajiwa kufungwa ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi katika maeneo yasiyofikika kirahisi na gridi ya taifa.
Mbali na hilo, amesema wakala unasaidia wazalishaji wadogo wa umeme wanaotumia maporomoko ya maji ili kuongeza matumizi ya nishati jadidifu na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyoharibu mazingira.
Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, REA inaendelea kufunga miundombinu ya majiko ya kisasa katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi zikiwemo shule, vyuo na taasisi za huduma za jamii.
Amesema katika awamu ya kwanza, pili na tatu za utekelezaji wa mradi huo, taasisi 454 zinazohudumia zaidi ya watu 100 zitafikiwa na miundombinu hiyo ambayo inafungwa bila gharama kwa taasisi husika.
Aidha, amesema REA inatoa ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na ruzuku ya asilimia 80 hadi 85 kwa majiko banifu ili kuwezesha wananchi wa vijijini kupata nishati safi kwa gharama nafuu.
Mha. Manyama amesema wakala umefunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza nchini na kambi 22 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zilizopo katika mikoa 14, hatua inayochangia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.










Post A Comment: