Articles by "REA"
Showing posts with label REA. Show all posts

📌Watumia fursa hiyo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia

Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), leo tarehe 24 Oktoba, 2026 wameshiriki mbio za Site Trust Marathon zilizofanyika wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Wakala zinazolenga kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Marathon hiyo imeandaliwa na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Juma Homera, kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa jamii katika shughuli za michezo na maendeleo.

Ushiriki wa REA katika marathon hiyo ni sehemu ya mkakati wa Wakala wa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ili kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia nchini.















 


“Tumebeba Matumaini ya Wananchi” — Mha. Saidy

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, amesema Serikali imedhamiria kukamilisha miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji vyote ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo itachochea shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Mha. Saidy ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Kikao Kazi cha Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kilicholenga kujadili utekelezaji wa majukumu, maendeleo ya miradi pamoja na kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha malengo ya Wakala yanafikiwa kwa wakati.

Akisisitiza umuhimu wa wajibu walio nao watumishi katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kufikisha nishati vijijini, Mha. Saidy amesema, “Tumebeba matumaini ya wananchi,” akiwataka watumishi kutambua kuwa mafanikio ya miradi yanagusa moja kwa moja maisha na shughuli za maendeleo za wananchi.

Aidha, Mha. Saidy amewataka wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu, sambamba na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika maeneo yao na kuhakikisha changamoto zinazoweza kuchelewesha miradi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesisitiza kuwa ushirikiano, ufuatiliaji madhubuti na uwajibikaji wa kila mtumishi ni muhimu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati, ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya umeme na kuitumia katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, REA inaendelea kuimarisha juhudi za Serikali za kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati vijijini, huku ikihimiza matumizi yenye tija ya umeme ili huduma hiyo iwe chachu ya kuinua uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo katika maeneo ya vijijini.










 


Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Bi. Martha Chassama, ameendelea kutoa elimu kwa vitendo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuandaa na kupika vyakula kwa kutumia majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za uelimishaji wa wananchi wanaotembelea banda la REA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya onesho hilo, Bi. Chassama amesema REA inaendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira, sambamba na kuboresha afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

“Nishati safi ya kupikia siyo tu suluhisho la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, bali ni uwekezaji katika afya za wananchi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa familia. REA inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu na fursa ya kutumia teknolojia hizi za kisasa ili kuboresha maisha yao,” amesema Bi. Chassama.

Amefafanua kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujionea kwa vitendo namna majiko ya kisasa yanavyofanya kazi, kufahamu manufaa yake pamoja na kupata elimu kuhusu teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia zinazotekelezwa na REA kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo.

Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kupunguza athari za kiafya zitokanazo na moshi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, pamoja na kuokoa muda na gharama zinazotumika katika kutafuta nishati za kupikia.

Bi. Chassama amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la REA ili kupata elimu kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, nishati safi ya kupikia na teknolojia za nishati jadidifu, zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuchochea maendeleo endelevu.

Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2026 yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, yakitoa jukwaa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha huduma, ubunifu na teknolojia zinazochangia maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa.










 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, leo Julai 14, 2026, amepokea tuzo ya Muoneshaji Bora wa Taasisi za Serikali (Government Institutions Exhibitor), ambayo REA ilitwaa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.

Tuzo hiyo imewasilishwa kwake na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Bi. Martha Chassama, kwa niaba ya watumishi walioshiriki katika maonesho hayo.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mha. Saidy amewapongeza watumishi wa Wakala kwa juhudi, kujituma na ushirikiano wao ulioiwezesha REA kutwaa tuzo hiyo.

Aidha, amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ushirikiano katika kutekeleza miradi ya REA vijijini na vitongojini, ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za nishati na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.



Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda ametembelea Maonyesho ya 50 Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam ikiwemo banda la Wakala wa Nishati Vijini (REA) na kuipongeza REA kwa uhamasishaji wa wananchi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia maeneo ya vijijini.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo Julai 2, 2026 baada ya kupata taarifa za miradi pamoja na kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Spika mtaafu Anna Makinda ameendelea kuhamasisha wananchi kutembelea banda la REA na kujifunza Teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia ili kuendelea kulinda mazingira pamoja na afya za wananchi.



 


Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia yapongeza utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Pongezi hizo zimetolewa leo Juni 24, 2026 na Mtendaji Mkuu wa REA Zambia, Mhandisi Alex Mbumba wakati wa ziara ya viongozi hao walipotembelea miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Vikonje Mkoani Dodoma.

“Tumekuja Tanzania kujifunza na kujionea namna miradi ya umeme vijijini inavyotekelezwa baada ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kufikisha umeme kwenye vijiji vyake vyote.

Tumekuwa na vikao na uongozi wa REA Tanzania toka tulivyowasili nchini kwa ajili ya kujifunza. Leo tumekuja kuona miradi ya umeme inavyotekelezwa na namna ilivyonufaisha na kuboresha maisha ya wananchi vijijini. Tumeona REA Tanzania inavyotekeleza miradi yake kwa ubora na viwango vya Kimataifa,” amesema Mhandisi Mbumba huku akiwahamasisha wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya kupeleka Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania, Mhandisi Deogratius Nagu amesema kuwa ujio wa ugeni huo kutoka REA Zambia ni ishara ya kutambuliwa kwa mafanikio yaliyofikiwa nchini katika kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi vijijini.

“Tanzania ni moja kati ya nchi chache Barani Afrika zilizofanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyake vyote, hivyo basi wenzetu wa Zambia wameona waje wajifunze ni kwa namna gani tumefanikiwa kutekeleza miradi yetu na kufikia mafanikio ya kufikisha umeme vijiji vyote vya Tanzania Bara,” amesema Mhandisi Nagu.












 


📌Washiriki Nishati Safi expo wafurahishwa na miradi ya REA

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeshiriki Maonesho na Kongamano la Nishati Safi expo 2026 yanayofanyika katika ukumbi wa Ubungo EACLC jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba. 

Akizungumza katika kongamano hilo leo Juni 24, 2026, Msimamizi wa miradi ya REA, Mha. Francis Manyama amesema kuwa, upatikanaji wa umeme vijijini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuongeza matumizi ya nishati safi.

Ameongeza kuwa, miradi ya usambazaji wa umeme vijijini imewezesha wananchi kuachana na matumizi ya majenereta na vyanzo vingine vya nishati vinavyotumia mafuta, hali inayosaidia kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.

Halikadhalika, REA inaendelea na mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua katika visiwa mbalimbali nchini, ambapo mifumo 20,000 inatarajiwa kufungwa ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi katika maeneo yasiyofikika kirahisi na gridi ya taifa.

Mbali na hilo, amesema wakala unasaidia wazalishaji wadogo wa umeme wanaotumia maporomoko ya maji ili kuongeza matumizi ya nishati jadidifu na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyoharibu mazingira.

Katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, REA inaendelea kufunga miundombinu ya majiko ya kisasa katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi zikiwemo shule, vyuo na taasisi za huduma za jamii.

Amesema katika awamu ya kwanza, pili na tatu za utekelezaji wa mradi huo, taasisi 454 zinazohudumia zaidi ya watu 100 zitafikiwa na miundombinu hiyo ambayo inafungwa bila gharama kwa taasisi husika.

Aidha, amesema REA inatoa ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na ruzuku ya asilimia 80 hadi 85 kwa majiko banifu ili kuwezesha wananchi wa vijijini kupata nishati safi kwa gharama nafuu.

Mha. Manyama amesema wakala umefunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza nchini na kambi 22 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zilizopo katika mikoa 14, hatua inayochangia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.