WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kukuza ubunifu, kuongeza bidii katika kazi, kutumia teknolojia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zilizo rafiki kwa Mazingira.

Mhe. Masauni amesema hayo katika Kongamano la Vijana lililofanyika jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026 ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo kilele chake kitaifa yanafanyika Juni 5, 2026 mkoani Dodoma.

Amesema, kongamano hilo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha vijana na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mijadala, kujifunza kutoka kwa wataalam, kubadilishana uzoefu na kuibua suluhisho bunifu zinazoweza kutekelezwa kwa vitendo katika jamii zao.

“Ninyi ndio nguvu kazi ya Taifa na nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana ni zaidi ya asilimia 64 ya nguvu kazi ya Taifa. Hii ina maana kuwa mchango wenu ni muhimu sana katika kulinda mazingira, kukuza uchumi wa kijani na kuhakikisha maendeleo endelevu ya Taifa letu.”

Aidha ameongeza kuwa ni vyema vijana wakatambua changamoto za kimazingira pia zinaweza kuwa fursa kubwa za kiuchumi, takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa mpito kuelekea uchumi wa kijani unaweza kuzalisha ajira milioni 8.4 kwa vijana duniani ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amesema uchumi endelevu duniani unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola trilioni 12 na uwezo wa kuzalisha zaidi ya ajira milioni 380 duniani kote.

“Hii inaonesha dhamira ya pamoja ya Taifa katika kulinda mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema kuwajengea uwezo vijana kupitia programu za kujitolea ni mkakati muhimu wa kuandaa kizazi kitakachosimamia agenda za maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na uchumi wa kijani.

Amesema programu za kujitolea zinawawezesha vijana kupata uzoefu wa kazi unaohitajika katika soko la ajira, huku zikizisaidia taasisi kupata kundi la vijana wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.

“Afrika ina hazina kubwa ya rasilimali watu, ambapo takribani asilimia 40 ya vijana wa dunia wanaishi katika bara hilo, jambo linalotoa fursa kubwa ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia endapo vijana hao watapatiwa elimu, ujuzi na nafasi za kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.” Amesema Dkt. Muyungi.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: