Serikali kupitia Wizara ya Fedha imetangaza vipaumbele vinane (8) vya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2026/27, vyenye lengo la kukuza uchumi, kuimarisha nidhamu ya matumizi ya rasilimali za umma, na kulipa madeni.
Vipaumbele hivyo vimewasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akisoma mapendekezo ya mpango na bajeti ya wizara hiyo.Sera na mikakati hiyo mikuu imegawanyika katika maeneo yafuatayo:
1. Ukuaji wa Uchumi na Kudhibiti Mfumuko wa BeiWizara imepanga kusimamia uchumi jumla ili ufikie ukuaji wa asilimia 6.3 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026. Aidha, jitihada zitawekwa ili kudhibiti mfumuko wa bei ubaki kwenye viwango vya tarakimu moja (wastani wa asilimia 3.0 hadi 5.0), huku akiba ya fedha za kigeni ikitunzwa kukidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa angalau miezi minne (4).
2. Nidhamu ya Matumizi na Ukusanyaji MapatoIli kuhakikisha thamani halisi ya fedha za umma inaonekana, serikali itaimarisha nidhamu ya bajeti (fiscal discipline). Hatua hii itahusisha usimamizi madhubuti wa ununuzi wa umma na kupunguza tabia ya kuhamisha fedha kutoka fungu moja kwenda jingine (reallocation between votes).
3. Kuvunja Rekodi ya Mapato (Tsh Bilioni 55,200.75)Katika bajeti kuu ya serikali ya jumla ya shilingi bilioni 62,334.19, Wizara ya Fedha inalenga kuboresha mifumo ya kodi, misaada, na mikopo ili kuchangia shilingi bilioni 55,200.75 kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Hii ni sawa na asilimia 88.6 ya bajeti yote.
4. Kulipa Madeni na Kuaminika KimataifaSerikali imetenga shilingi bilioni 15,102.80 kwa ajili ya kulipa kwa wakati riba na mitaji ya madeni yanayotarajiwa kuiva. Hatua hii inalenga kulinda mikataba na kuendelea kujenga imani kwa wawekezaji katika masoko ya fedha ya kikanda na kimataifa.
5. Mabilioni ya Kulipa Watumishi na WakandarasiHabari njema kwa wadau wa ndani ni kwamba serikali itakuwa ikitoa shilingi bilioni 100.00 kila mwezi. Fedha hizi zitasaidia kulipa madeni ya watumishi wa umma, wakandarasi, wazabuni, na watoa huduma mbalimbali ili kuchochea mzunguko wa fedha.
6. Usawa wa Mgawanyo wa Fedha kwa HalmashauriKutakuwa na maboresho makubwa kwenye ugawaji wa rasilimali fedha kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa (Halmashauri). Mgawanyo huo utazingatia tafiti za kitaalamu ili kuondoa urudufu wa majukumu na kuleta uwiano wa kimaendeleo nchini.
7. Mageuzi ya Mfumo wa Bajeti (PBB)Serikali itafanya tathmini ya kina ya usimamizi wa bajeti kwa kutumia Mfumo wa Programu (Programme Based Budgeting – PBB). Lengo ni kuwezesha maamuzi sahihi ya kimabadiliko katika upangaji wa bajeti unaoleta matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.
8. Matumizi ya Akili Unde (AI) na Utawala BoraKatika kwenda na wakati, wizara itajenga uwezo wa watumishi wake kuhusu masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG). Kubwa zaidi, serikali itaanza kuingiza matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) katika usimamizi wa fedha za umma na uchumi ili kuongeza ufanisi na uwazi.

Post A Comment: