Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuipa nafasi pana sekta binafsi kushiriki katika ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ajira kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), wakati akihutubia katika hafla ya Ufungaji wa Maonesho ya Nne ya Biashara ya Mbeya City Expo yaliyodumu kwa siku tisa Mei 30, 2026 jijini Mbeya.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), Mhe. Londo amebainisha kuwa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuweka msisitizo katika uwekezaji wa rasilimali watu, teknolojia, na ubunifu huku akisisitiza kuwa kujenga taifa lenye wananchi wanaojitegemea kiuchumi ndio msingi thabiti wa maendeleo endelevu ya nchi.
Londo ameeleza kuwa Wizara kupitia Taasisi zake ikiwemo SIDO, ina programu maalum za kuwanoa vijana na wajasiriamali katika nyanja za elimu ya Ujasiriamali, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, na masoko kwa lengo la kukuza mnyororo wa thamani kuanzia viwanda vidogo, vya kati, hadi vikubwa ili kuongeza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) ukishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa maandalizi mazuri yaliyofanikisha maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya "Kujenga Uchumi wa Kikanda Kupitia Biashara na Uwekezaji".
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mhe. Jaffar Haniu akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesema Maonesho hayo yanalenga kukuza uwekezaji, biashara na maslendeo ya uchumi ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
















Post A Comment: