Mbunge wa Tunduru Kaskazini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amewataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuepuka kuingiza siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 katika mijadala ya Bunge, akisema hali hiyo inaweza kuathiri ubora wa majadiliano na utekelezaji wa majukumu muhimu ya chombo hicho.


Akichangia hoja ya Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Juni 2, 2026, Bungeni jijini Dodoma, Ado amesema Bunge ni taasisi muhimu inayopaswa kujadili masuala ya maendeleo kwa umakini bila kuruhusu ushindani wa kisiasa kutawala kila mjadala.

"Nafahamu siasa zinaendeshwa na siasa, na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sehemu ambayo siasa haziwezi kuepukika. Hata hivyo, nawaomba wabunge wa CCM, homa ya kuelekea mwaka 2030 isiharibu mijadala ya Bunge hili," alisema.

Ameongeza kuwa ingawa siasa zina nafasi yake, kuzidisha mijadala ya kisiasa mapema kunaweza kuondoa mwelekeo wa Bunge katika kushughulikia masuala ya msingi yanayogusa maendeleo ya wananchi.

"Kuna ladha katika siasa, lakini tukizidisha chumvi mapema kiasi hiki, tutafika mahali ambapo hakuna wizara itakayoweza kujadiliwa kwa utulivu ndani ya Bunge. Mwenendo huo si mzuri kwa ustawi wa Bunge la Muungano wa Tanzania," alisisitiza.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa kazi iliyoifanya katika kupitia masuala ya fedha za Serikali, sambamba na kupongeza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuendelea kusimamia uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Ado amesema mafanikio ya maendeleo ya taifa yanategemea uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma, hivyo akaishauri Serikali kuendelea kuipatia Ofisi ya CAG rasilimali na fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

"Endapo tutaamua kuwa makini na kutekeleza wajibu wetu ipasavyo, nchi inaweza kufikia hatua kubwa zaidi za maendeleo. Ni muhimu Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali

(CAG)ikawezeshwa vya kutosha ili iendelee kufanya kazi yake kwa uhuru na ufanisi," amesema.

Kauli za Ado zimekuja wakati Bunge likiendelea kujadili bajeti za wizara mbalimbali kuelekea mwaka wa fedha 2026/2027.

Share To:

Post A Comment: