Na Mwandishi Wetu
Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na Wakala wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL) wamesaini ya kuwatafutia fursa mbalimbali za kilaaluma wanafunzi a chuo hicho.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel na kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Pendo Malangwa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, mgeni rasmi ambaye alimwakilisha Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Kituye aliipongeza GEL na DUCE kwa kuona umuhimu wa kuingia makubaliano hayo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza sana DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kusaidia maendeleo ya elimu na maandalizi ya vijana wetu kwa maisha ya kazi baada ya hatua mbalimbali za masomo,” alisema Kituye.
Aidha, alisema Dar es Salaam ni mkoa wenye nafasi kubwa sana katika maendeleo ya taifa kwani una idadi kubwa ya ya watu, shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi, vyuo vya elimu ya juu, hospitali za rufaa na za binafsi, pamoja na viwanda vikubwa na vya kati vinavyoendelea kukua kila siku.
Alisema ukuaji huo wa uchumi na miundombinu una maana moja kubwa sana kwa wadau wa elimu kwani unamaanisha kuna wajibu wa kuandaa vijana wenye maarifa, ujuzi, maadili, na uwezo wa kutumia fursa zinazozidi kuongezeka katika mkoa huo na taifa.
“Ndiyo maana suala la kunasihi vijana kuhusu ulimwengu wa kazi baada ya masomo lina umuhimu mkubwa sana katika kipindi hiki. Kimsingi, mwanafunzi wa leo anatakiwa kujitambua mapema hususani kuelewa uwezo wake, mahitaji yake, ndoto zake, na fursa za kazi zilizopo mbele yake,” alisema .
Alisema kijana anatakiwa kusoma akiwa anajua anasoma nini, kwa nini, na anakwenda kutumia vipi maarifa na ujuzi alioupata.
Alisema bila mwongozo sahihi wa taaluma, vijana wengi wanaweza kuchagua masomo bila kulinganisha matamanio yao, uwezo wao na mahitaji ya soko la ajira au fursa zinazokuja katika miaka ijayo.
“Kwa kuzingatia hilo, ni jambo la faraja kuona kuwa DUCE pamoja na Global Education Link wameamua kuunganisha nguvu katika eneo hili muhimu,” alisema.
“Kwa niaba ya Ofisi ya Elimu Mkoa wa Dar es Salaam napenda kuupongeza tena uongozi wa DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuanzisha ushirikiano huu muhimu. Ni imani yangu kuwa hatua hii ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika namna tunavyowaandaa vijana wetu kwa elimu, ajira, ubunifu, na maisha ya baadaye,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel alisema GEL imefikisha miaka 19 katika kufanyakazi ya kuwapa wanafunzi mwongozo wa taaluma za kusomea.
Alisema kazi kubwa ambazo wanafanya ni kuwatafutia wanafunzi wa Tanzania kupata fursa za kusoma nje ya nchi na kusaidia ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya ndani nan je ili kuchukua teknolojia kwenye nchi hizo.
Alisema nchi zilizoendelea zimefika hapo kutokana na maarifa makubwa ya wananchi wake hivyo GEL imeona umuhimu wa kuchukua maarifa hayo yaje kusaidia hapa nchini Tanzania.
Alisema GEL imesaini mikataba kama hiyo na vyuo vikuu vya Dodoma, Mzumbe, Nelson Mandela, TIA na vingine na kwamba kusaini na DUCE ni mwendelezo wa utaratibu huo.
“Kila chuo tunachosaini makubaliano tunakuwa na malengo maalum nacho, leo tumesaini na DUCE kwaajili ya mwongozo kwa wanafunzi na hatuishii kwa wanafunzi, wazazi ambao wanataka kujiendeleza kielemu au walimu wanaotaka kujiendeleza tunawapa mwongozo,” alisema Mollel
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Pendo Malangwa alisema tukio hilo linaonyesha dhamira ya dhati ya kuwaaandaa vijana kwenye maisha ya taaluma na hatimaye ajira siku za baadae.
Alisema kupitia ushirikiano huo wanafunzi wa chuo hicho watapata mwongozo wa kitaaluma na kuelewa fursa zilizoko ndani nan je ya nchi kwaajili ya kupambana na ushindani unaokua kwa kasi ulimwenguni kwenye soko la ajira.
Alisema DUCE inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa elimu bora, kufanya tafiti na kuandaa wataalamu na kwamba GEL itaweka uzoefu wake kwa kuwaunganisha vijana kwa kuwapa ushauri na maendeleo ya kitaaluma.
Tunatarajia kuongeza mwongozo wa kitaaluma na ushirikishwaji wa wanafunzi na kuwajengea uwezo na kuimarisha mawasiliano kupitia vyombo vya habari ili kusaidia vijana kuelewa taaluma mbalimbali na mahitaji ya soko la ajira.
“Sote ni mashahidi hapa vijana wengi wakimaliza kidato cha sita hawana uwezo wa kuchagua wanachotaka kusoma, wengine wanachagua tu kwasababu walisikia, sasa kupitia ushirikiano huu tunataka vijana wachague kitu wanachokijua kitakacholeta tija kwenye maisha yao ya baadae,” alisema










Post A Comment: