NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuhakikisha wafanyabiashara wa Kariakoo wanakuwa na ushindani wa kikanda na kimataifa huku ikiitaja Kariakoo kuwa moyo wa biashara wa Tanzania na injini muhimu ya uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa leo Mei 17, 2026 katika hafla ya Utoaji wa Tuzo za Biashara Kariakoo ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, amesema Kariakoo si eneo la kawaida katika historia ya biashara nchini bali ni alama ya uchapakazi, uthubutu na mafanikio ya Watanzania wengi.

Amesema Kariakoo imekuwa sehemu iliyojenga maisha ya maelfu ya wananchi, huku vijana wengi wakianza biashara kwa mitaji midogo na baadaye kuwa waajiri wakubwa.

“Kila siku maelfu ya watu wanaingia Kariakoo kufanya biashara, kununua bidhaa, kuwekeza na kusafirisha bidhaa kwenda ndani na nje ya nchi ikiwemo DRC, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Uganda na Comoro,” amesema.

Mbwasi amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya biashara, uwekezaji na viwanda ili wafanyabiashara waweze kushindana katika soko la kimataifa.

Akizungumzia ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo baada ya janga la moto, amesema Serikali ilihakikisha soko hilo linajengwa upya kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo mradi huo uligharimu takribani shilingi bilioni 28 na kuwa na zaidi ya maduka 2,000.

Amesema Serikali inaamini sekta binafsi ni mshirika mkuu wa maendeleo ya uchumi, ndiyo sababu imeendelea kuboresha mazingira ya biashara, kurahisisha uwekezaji, kupanua miundombinu ya masoko na kuimarisha huduma za kidigitali.

Aidha, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha wanapata mazingira yenye utulivu, uwazi na usalama wa mitaji yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kariakoo Business Awards, Zakayo Shushu, amesema tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kutambua ubunifu, uwekezaji na juhudi za wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa uaminifu na weledi mkubwa.

Amesema tuzo hizo zinalenga kukuza biashara zinazoaminika pamoja na kuchochea ushindani wa kitaalamu ili wafanyabiashara wa Kariakoo waweze kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.

“Tunataka kujenga mazingira ya ushindani wa kimataifa na kuhakikisha wafanyabiashara wetu wanakuwa sehemu ya ushindani mkubwa wa biashara duniani,” amesema.

Shushu ameongeza kuwa ajenda nyingine muhimu ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuhakikisha sauti ya mlaji inasikilizwa na kuthaminiwa.

Amesema kwa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi, wamepanga kuanzisha majukwaa mbalimbali yatakayoinua Kariakoo pamoja na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

Aidha, amebainisha kuwa kuna mikakati ya kuanzisha mafunzo kwa wafanyabiashara pamoja na kampeni maalumu za kuitangaza Kariakoo duniani kama kitovu muhimu cha biashara.

Amesema maboresho ya miundombinu ya biashara, mazingira ya uwekezaji pamoja na utatuzi wa changamoto za wafanyabiashara yameendelea kuongeza imani ya wafanyabiashara kwa Serikali yao.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: