Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika sekta ya elimu ya juu kwa lengo la kukuza ubora wa elimu, kubadilishana maarifa na kuendeleza lugha ya Kiswahili pamoja na taaluma mbalimbali nchini.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kimataifa wanaosoma katika vyuo vikuu vya Tanzania kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha diplomasia ya elimu na kukuza nafasi ya nchi katika ramani ya elimu duniani.
“Serikali itaendelea kuwafadhili wanafunzi 15 raia wa China wanaosoma Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hatua inayolenga kukuza na kubiasharisha Kiswahili kimataifa. Aidha, wanafunzi wawili raia wa Oman pamoja na wanafunzi watano raia wa Hungaria wataendelea kusoma katika vyuo vikuu vya Tanzania kwa kuzingatia mikataba na taratibu za ushirikiano wa elimu ya juu.”amesema
Hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kitamaduni kati ya Tanzania na mataifa mengine, sambamba na kuongeza mvuto wa vyuo vikuu vya nchini kama kituo cha kimataifa cha elimu.
Katika upande mwingine, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vikuu na taasisi za sayansi na teknolojia kwa kuwekeza katika miundombinu muhimu ya elimu. Hii ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa vyumba vya semina, kumbi za mihadhara, madarasa, ofisi, maabara, maktaba pamoja na miundombinu mingine ya kitaaluma.
Utekelezaji wa maboresho hayo unafanyika katika taasisi 21 za elimu ya juu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, hatua inayolenga kuongeza ubora wa elimu, utafiti na ubunifu ili kuchochea maendeleo ya taifa.
Serikali imeeleza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha elimu ya juu na utafiti barani Afrika, huku ikituza matumizi ya Kiswahili na kuongeza ushindani wa wahitimu wake katika soko la ajira la kimataifa.


Post A Comment: